Serikali imeendelea kujitetea kuhusu mpango wa uagizaji wa mafuta wa serikali kwa serikali maarufu kama G to G, huku viongozi wa kisiasa wakitoa mitazamo kinzani kuhusu utekelezaji wake.
Serikali kupitia Mamlaka ya kudhibiti bei za mafuta nchini EPPRA, imetangaza ongezeko la bei mpya za mafuta kwa shilingi 28 kwa lita moja ya mafuta ya petrol huku diseli ikiongezeka kwa shilingi 40 kwa lita.
Hatua hii imezua mjadala mkali kuhusu athari za mfumuko wa bei nchini.
Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Kinara wa Chama cha DCP, Rigathi Gachagua, na Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka wamekosoa vikali serikali kufutia ongezeko la bei ya mafuta wakisema mpango wa G to G ilikuwa ni njama ya kumfaidi Rais William Ruto, wakifichua kwamba takriban shilingi tano kwa kila lita ya mafuta itakayouzwa nchini itakuwa inamfaidi Rais Ruto.
Viongozi hao pia, walimtaka Waziri wa Kawi na Petroli nchini Opiyo Wandayi, pamoja na Waziri wa Biashara na Uwekezaji wa viwanda nchini Lee Kinyanjui, kujiuzulu.
Kwa upande wake mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro pia ameukosoa mpango huo akidai kwamba ni njama ya baadhi ya viongozi wakuu serikalini kujinufaisha binafsi.
Nyoro aliema mpango huo ni njia ya kuwahadaa wakenya ilhali mzigo mkubwa unaishia kwa walipa ushuru.
Aliongeza kuwa mpango huo unanufaisha baadhi ya kampuni za mafuta nchini zinazodaiwa kumilikiwa na viongozi wa juu serikalini huku akitoa baadhi ya mapendekezo kwa serikali pamoja na wadau wa sekta ya kawi ambayo kulingana naye, yanaweza kushusha bei ya mafuta kwa takriban shilingi 27.
Hata hivyo, Rais William Ruto ametetea mpango huo akisema serikali imetumia takriban shilingi bilioni 6.5 kutoa ruzuku ya mafuta ili kupunguza mzigo kwa wananchi hasa ushuru wa VAT kwa asilimia 8.
Kwa upande wake, Waziri wa Kawi na Petroli nchini Opiyo Wandayi alisema serikali imejizatiti kukabiliana na wanaojihusisha na uagizaji wa mafuta ghushi humu nchini.
Hata hivyo, kumeshuhudiwa tofauti katika takwimu za fedha zilizotolewa kuhusu mpango huo, Rais akitaja bilioni 6.5 ilhali Waziri Wandayi akisema serikali iliwekeza takriban bilioni 6.2.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
