Wakenya wanaojitokeza kujisajili kama wapiga kura katika zoezi endelevu lililoidhinishwa na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, inatia matumaini ya Tume hiyo kufikia malengo yake ya kusajili wa idadi ya watu milioni 6.2 kote nchini.
Katika kaunti ya Kilifi kwenye eneo bunge la Kilifi Kazkazini ambapo zoezi hilo linaendelea, Maafisa wa Tume hiyo wamedai kupitia changamoto wakati wa usajali wa wapiga kura.
Maafisa hao wanasema kati ya changamoto hizo ni pamoja na kuitishwa pesa na vijana ndipo wawasajili kuwa wapiga kura, wakisema changamoto hiyo inarudisha nyuma juhudi zilizoidhinisha na Tume ya IEBC.
Afisa anayesimamia Tume ya IEBC katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini John Mwawasi alisema licha ya changamoto hizo, kufikia sasa maafisa wa tume hiyo wanaozuru nyanjani wamefanikiwa kusajili wapiga kura wapya kwa asilimia 50.
Mwawasi alisema japo wanalenga kusajili idadi ya wakenya zaidi ya elfu 13 katika eneo bunge hilo, kufikia sasa wamesajili wakenya zaidi ya elfu 6.
“Changamoto ambayo tunapitia kwa sasa ni vijana ambao tunalenga kuwasajili wamekuwa wakiitisha pesa maafisa wetu ili wasajiliwe kuwa wapiga kura wapya lakini tumekuwa tukiwaeleza kwamba zoezi hili ni hiari na kwamba litawapa nafasi nzuri ya kufanya mabadiliko ya kiuongozi kuanzia ngazi ya kitaifa hadi mashinani”,alisema Mwawasi.
Wakaazi waliokuwa wamefika katika ofisi za IEBC kusajiliwa wameelezea wepesi wa zoezi hilo, kutokana na maafisa hao wanatumia mfumo wa kieletronic.
Tume hiyo ya IEBC imejitenga na masuala ya kujihusisha na siasa na kuwarai wanasiasa kuwasaidia katika kuwarai wananchi hasa vijana kujisajili kama wapiga kura, kauli ambayo imeungwa mkono na Naibu Mwenyekiti wa IEBC Fahima Araphat.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi