Tume ya huduma za Mahakama nchini JSC imetangaza kupokea maombi ya wakenya wanaotaka kujaza nafasi iliyowachwa wazi ya Jaji wa Mahakama ya Upeo Mohammed Ibrahim.
Katika notisi iliyochapishwa na Tume hiyo, ilisema tangu tangazo la nafasi hiyo kuwekwa wazi, ni wakenya 6 pekee waliotuma maombi ya kutaka kushikilia wadhfa huo kabla ya tangazo hilo kufungwa rasmi Februari 17 mwaka huu.
Wakenya waliotuma maombi ya kujaza nafasi hiyo ni pamoja na Jaji Warsame Abdulahi Mohammed, Jaji Joseph Kiplagat Sergon, Jaji Joseph Kipchumba Katwa Kigen, Jaji Francis Kipruto Tuiyott, Ann Waceke Kiratu Makori na Lilian Wanjiku Wachira.
Tume hiyo JSC ilisema inapanga kuandaa kikao cha washikadau mwezi Machi 23 mwaka huu ili kujadili jinsi watakavyoandaa zoezi la kuwapiga msasa wale watakaoorodheshwa kuwania nafasi hiyo.
Notisi hiyo pia ilieleza kwamba Tume ya JSC itatoa tarehe maalum ya zoezi la kuwapiga msasa wakenya hao ambalo litafanywa wazi ili wananchi waweze kufuatilia zoezi hilo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
