Maraga aishutumu serikali kwa kuendeleza ufisadi

Maraga aishutumu serikali kwa kuendeleza ufisadi

Jaji mkuu mstaafu David Maraga ameishtumu serikali ya kitaifa kwa kuendeleza ufisadi kupitia miradi hewa nchini.

Akizungumza wakati wa mikutano yake ya kisiasa katika kaunti ya Taita taveta, Maraga alisema  sakata ya ufisadi ya shilingi bilioni 11 kwa uwanja wa talanta ni ishara wazi kwamba serikali ya Kenya kwanza imesheheni ufisadi.

Maraga ambaye alitangaza nia yake ya kuwania wadhfa wa urais wakati wa uchaguzi mkuu ujao, alielezea kushangazwa na jinsi maafisa wa umma wanavyopora mali ya umma.

Aidha aliahidi kujitolea kupambana kikamilifu na ufisadi nchini iwapo wakenya watamchagua kama rais mwaka wa 2027.

Maranga ambaye pia ni Kinara wa chama cha United Green Movement UGM alirejelea suala la raslimali zilizopo katika kaunti ya Taita Taveta hasa madini akisema hazijawanufaisha wakaazi wa kaunti ya Taita Taveta ipasavyo kutokana na ufisadi.

Vile vile alilitaka Shirika la kulinda na kuhifadhi wanyamapori KWS kuingilia kati na kuhakikisha mzozo baina ya wakaazi wa kaunti hiyo na wanyamapori unatatuliwa.

Taarifa ya Elizabeth Mwende