Kesi ya ulaghai wa shilingi milioni 1.2 inayomkabili mshukiwa Emmanuel Kithi imewasilishwa katika Mahakama ya Kilifi.
Mshukiwa Emmanuel Kithi anadaiwa kumlaghai mlalamishi Moses Mwafondo kwa kumuahidi kwamba atampea zabuni ya usambazaji wa bidhaa mbalimbali kwa Manuspaa ya Malindi zenye thamani ya shilingi 1,205,598.
Katika kesi hiyo iliyowasilishwa Mahakamani, mshukiwa Kithi inadaiwa kutekeleza kitendo hicho kati ya tarehe tofauti mnamo mwezi Disemba mwaka 2024 na mwaka 2025.
Hakamu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa alimnyima dhamana mshukiwa huyo pamoja na kuagiza kuzuiliwa rumande katika gereza la Kilifi, kaunti ya Kilifi.
Hakimu Obulutsa aliagiza mshukiwa kurejeshwa tena Mahakamani mnamo tarehe 25 mwezi Februari mwaka huu ambapo Mahakama itatoa uamuzi wa iwapo mshukiwa atapewa dhamana au la.
Hii ni baada ya upande wa ashtaka kupinga ombi lililowasilishwa na Wakili wa mshukiwa la kutaka Mahakama ilimuachilie kwa dhamana mteja wake baada ya kubainika kwamba ni mfanyikazi wa serikali ya kaunti ya Kilifi katika Idara ya jinsia, pamoja na kubainika kwamba amekuwa akitekeleza vitendo hivyo vya ulaghai kwa watu wengine.
Mshukiwa huyo hata hivyo alikanusha mashtaka dhidi yake, licha ya Mahakama kubaini kwamba jamaa huyo ana kesi nyingine ya kujibu ya shilingi milioni 1.6 katika Mahakama hiyo.
Taarifa ya Teclar Yeri
