Business
Wavuvi wa Kilifi wanalalamikia ukiukaji wa sheria za kuvua samaki

Wavuvi kutoka eneo la Old Ferry wanadai kuna baadhi ya wavuvi ambao wanatumia nyavu ambazo zilipigwa marufuku.
Kulingana na wavuvi, Nyavu hizo zinavua hadi samaki wadogo na kuharibu maeneo ya samaki ya kuzaana hali ambayo inasababisha kupungua kwa idadi ya samaki baharini.
Wakiongozwa na James Kahindi, Wavuvi hao walisema sekta ya uvuvi imedorora kutokana na upungufu wa samaki kwani vifaa wanavyotumia ni hafifu na haviwezi kuvua katika maji makuu.
Wakizungumza na Coco Fm, Wavuvi hao walitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Kilifi kuwawezesha wavuvi kifedha na hata kuwapa vifaa vya kisasa ili kuweza kuvua samaki kwenye maji makuu
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
KPA kushirikiana na kaunti ya Siaya kibiashara

Halmashauri ya bandari Kenya (KPA) pamoja na serikali ya kaunti ya Siaya zimeahidi kushirikiana kwa karibu kuimarisha miundomsingi ya usafiri na biashara katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Katika kikao cha viongozi wa pande zote mbili kilichofanyika jijini Mombasa, viongozi hao walijadili miradi ya miundomsingi ya baharini inayolenga kufungua fursa mpya za uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ya Ziwa Victoria.
Mkurugenzi mkuu wa KPA nahodha William Ruto alithibitisha kuwa usanifu wa kivuko cha Usenge utakamilika ndani ya wiki mbili, huku ikiahidi kushirikiana na Kenya Shipyards Limited kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati.
Aidha, Ruto alieeleza utayari wa mamlaka hiyo kushirikiana na serikali ya kaunti ya Siaya kuhakikisha miradi hiyo inaendana na vipaumbele vya eneo hilo.
Ruto aliongeza kuwa miradi hiyo inalenga kuchochea uwekezaji, kuongeza nafasi za ajira na kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika ukanda wa ziwa.
Kwa upande wake, gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo alieleza kuridhishwa na ushirikiano huo, akimpongeza nahodha Ruto kwa uongozi wake wa vitendo akisema kuwa miradi hiyo inaleta matumaini mapya kwa wakazi wa Siaya na ukanda mzima wa Ziwa Victoria.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
Business
Wadau wa sekta ya uvuvi walalamikia unyakuzi wa ardhi

Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu uchumi wa bahari na masuala ya ubaharia imewataka wawekezaji wote waliovamia ardhi zilizotengewa
Kauli hii ilijiri baada ya wavuvi na wasimamizi wa fuo za bahari kuelekeza lalama zao kwa kamati hiyo wakidai kuhangaishwa kila mara na baadhi ya mabwenyenye wanaodaiwa kushirikiana na baadhi ya maafisa wa serikali.
Walidai kwamba unyakuzi huo umekuwa donda sugu na uliadhiri pakubwa shughuli za uvuvi huku wakiitaka serikali ya kitaifa kuingilia kati na kuhakikisha ardhi hizo zinarudhishwa mikononi mwa jamii za wavuvi haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo na ambaye pia ni mbunge wa Marakwet Mashariki David Kangogo Bowen alisema ujenzi wa kibinafsi katika maeneo ya mita 60 kutoka ukingo wa bahari ni ukiukaji wa sheria kwani maeneo hayo yametengwa mahususi kwa matumizi ya wavuvi.
“Wale wamejenga mita 60 kando ya bahari waondolewa ndio hawa wavuvi wapewe nafasi ya kufanya biashara yao vizuri na pia wapate sehemu ya kuegeza maboti yao”. … alisisitiza David Bowen.
Kauli yake iliungwa mkono na mbunge wa Matunga Kassim Sawa Tandaza aliyesema agizo hilo ni sharti litekelezwa mara moja na yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Taarifa ya Elizabeth Mwende