News
Watu wawili wafariki kutokana na Mpox Mombasa

Serikali ya kaunti ya Mombasa imethibitisha vifo vya watu wawili kutokana na ugonjwa wa Mpox, huku maambukizi mapya yakiendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
Msimamizi mkuu wa Idara ya afya kaunti ya Mombasa, Dkt Mohammed Hanif, alisema tangu ugonjwa wa Mpox uripotiwe humu nchini Julai 31, 2024, jumla ya visa 226 vimeripotiwa ikiwemo vifo 4, huku kaunti ya Mombasa ikiwa miongoni mwa kaunti 21 zilizoathirika.
Dkt Hanif alisema kisa cha kwanza cha Mpox kaunti ya Mombasa kiliripotiwa Septemba 3, 2024, na kufikia sasa watu 159 wamefanyiwa vipimo, ambapo 98 kati yao wamethibitishwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza na Wanahabari, Dkti Hanif alisema kati ya wagonjwa hao, 24 wamelazwa katika kituo cha kutenga na kutibu wagonjwa katika kituo cha afya cha Coast General eneo la Utange huku akisema kumekuwa na ongezeko la maambukizi mapya mwezi ya Juni na Julai.
“Hii ugonjwa iko na tayari watu 159 wamefanyiwa vipimo ambapo 98 kati yao wamethibitishwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo na kati ya wagonjwa hao, 24 wamelazwa katika kituo cha kutenga na kutibu wagonjwa katika kituo cha afya cha Coast General eneo la Utange”, alisema Dkt Hanif.
Kwa upande wake, Afisa wa Shirika la Stawisha Pwani, Vinceny Omoth, aliwataka wakenya hususan wale wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Wahudumu wa afya Lamu watishia kuishtaki serikali ya kaunti hiyo

Wahudumu wa Afya kaunti ya Lamu wametishia kuelekea Mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti hiyo kwa kukaidi kutekeleza matakwa yao.
Wahudumu hao waliishtumu serikali ya kaunti ya Lamu kwa kupuuza matakwa yao na badala yake kutumia vitisho ili kuwashurutisha kurejea kazini.
Kulingana na viongozi wa wahudumu hao, licha ya mgomo wao kuendelea kwa zaidi ya wiki mbili serikali ya kaunti hiyo imekataa kata kuandaa vikao vya kusuluhisha malalamishi yao.
Baadhi ya changamoto wanazolalamikia ni pamoja na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kupandishwa vyeo, kupuuzwa kwa mkataba wa makubaliano ya nyongeza ya mishahara, kunyimwa kwa mishahara kwa baadhi ya wahudumu hao miongoni mwa matakwa mengine.
“Mkiendelea kutufinyilia itabidi tufuate njia ya sheria kwa sababu tunajua tunalilia haki yetu, haiwezekani serikali ya kaunti inashindwa kutupandisha vyeo ilhali tumefanya kazi kwa miaka 15 sasa, hatuwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira duni na pia mkataba wa makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara sharti itekelezwe” walisisitiza viongozi hao.
Wakati uo huo serikali ya kaunti ya Lamu imejibu malimishi yao kupitia barua na kutangaza kuwa mgomu huo ni kinyume cha seria na kuwataka wahudumu hao kurejea kazini mara moja.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Rais Ruto atuma KDF kusimamia ujenzi wa hospitali nchini

Rais William Ruto ametuma jeshi la KDF kusimamia ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 75 kote nchini katika juhudi za kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa haraka.
Akizungumza katika kaunti ya Narok wakati wa uzinduzi wa hospitali ya Sogoo Level 4, waziri wa ulinzi Patrick Mariru alifichua kuwa ujenzi wa hospitali hiyo yenye mamlaka kamili itakamilika baada ya mda wa miezi 11.
Ujenzi wa hospitali ya Sogoo Level 4 ulivutia rais Ruto alipozuru eneo hilo mwezi mei mwaka 2025, jambo lililomfanya kuagiza KDF kuipandisha hadhi.
Mariru hata hivyo alishikilia kuwa wafanyikazi wote wasio na ujuzi watatolewa kutoka kwa jamii.
“Jeshi litamsimamia mkandarasi. Hilo liwe wazi, kazi yote itafanywa na vijana wa Sogoo. Tutaweka maafisa wawili na kila jioni watanipa ripoti ya maendeleo,” alisema Mariru.
“Tuna zaidi ya miradi 75 tunayosimamia na sio kwamba tunabadilisha wakala wa serikali tunataka tu kushirikiana na ofisi tofauti miongoni mwao wizara za afya na michezo.”
Taarifa ya Joseph Jira