News
Walimu 294 wa shule za chekechea wamepandishwa vyeo Taita Taveta

Jumla ya walimu 294 wa shule za chekechea kaunti ya Taita Taveta wamepandishwa vyeo kulingana na kiwango chao cha masomo yao.
Akiwahutubia walimu hao gavana wa kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime alisema hatua hiyo inalenga kuboresha utendakazi sawa na kuwatia motisha baada ya juhudi zao kukosa kutambuliwa kwa mda mrefu.
Hata hivyo Mwadime aliwataka walimu hao kuwajibika zaidi katika maeneo yao ya kazi, akitaja sekta ya elimu kuwa nguzo muhimu katika ujenzi wa jamii bora na iliyo na maadili.
“Mlikuwa mnafanya kazi kwa muda mrefu, mlikuwa mnafundisha, mwalipwa elfu tatu, saa ingine mwaenda bila mshahara.Hamna aliyemtambua hapo awali’’, alisema Mwadime.
Ni Kauli iliungwa mkono na naibu gavana wa kaunti hiyo Christine Kilalo ambaye aliwahimiza walimu hao kuwafunza watoto ipasavyo ili viwango vya elimu kwenye kaunti hiyo viweze kuimarika hata zaidi.
Walimu waliopandishwa cheo ni kati ya walimu 697 wanaofundisha katika shule mbalimbali za chekechea kaunti ya Taita Taveta.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Gachagua atangaza azma ya kuwania urais 2027

Kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua ametangaza nia ya kuwania wadhfa wa urais mwaka 2027 akilenga kumg’oa rais William Ruto mamlakani.
Gachagua amekuwa akifanya ziara katika eneo la mlima kenya pamoja na viongozi wa chama chake akitumia mikutano ya barabarani kutangaza azma yake ya kuwania urais.
Kulingana na Gachagua serikali ya sasa inatumia mikutano ya ikulu kuendeleza vitendo vya ufisadi, na ameahidi kuwa akichaguliwa atakomesha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika ziara hiyo viongozi wa chama chake walieza kuwa Gachagua ndiye mgombea anayefaa kupeperusha bendera ya upinzani, wakidai eneo la mlima kenya limejiondoa katika uungwaji mkono wa serikali ya sasa.
Taarifa ya Joseph Jira.