Business
Wakulima wa Mwani Kwale Waitaka Serikali Kulitambua Zao Lao

Washikadau wa sekta ya kilimo cha mwani katika Kaunti ya Kwale wametoa wito kwa serikali kuu kulitambua rasmi zao hilo kama zao la kibiashara, ili kuwasaidia wakulima kunufaika zaidi kiuchumi.
Mshirikishi wa mradi wa mwani katika shirika la Plan International, Bw. Alfred Rono, amesema kuna haja ya kuundwa kwa sera mahsusi zitakazowalinda na kuwawezesha wakulima wa mwani kupata masoko ya uhakika na kuongeza thamani ya mazao yao.
Akizungumza katika eneo la Mkunguni, Msambweni, Bw. Rono amesema mwani una uwezo mkubwa wa kuchangia mapato ya wakulima wadogo na kukuza uchumi wa eneo hilo iwapo utawekewa mazingira wezeshi ya uzalishaji na usambazaji.
Kauli yake imeungwa mkono na Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Bahari na Uvuvi (KMFRI), Bw. Anthony Nzioka, ambaye ametoa wito kwa serikali kuu kulijumuisha zao la mwani katika orodha rasmi ya mazao ya kibiashara nchini.
Business
Mvua Yawaathiri Wafanyikazi wa Fuo za Bahari Mombasa

Wafanyikazi wa fuo za bahari katika Kaunti ya Mombasa wamelalamikia athari za mvua zinazoendelea kunyesha, wakisema hali hiyo imepunguza shughuli zao za kila siku na kuathiri mapato yao.
Wakizungumza na vyombo vya habari, wafanyikazi hao wamesema kuwa mvua kubwa iliyoshuhudiwa katika kipindi hiki imechangia kupungua kwa idadi ya watalii wanaotembelea fuo hizo, hali ambayo imesababisha kupungua kwa kipato chao.
Aidha, wamesema kuwa bahari kwa sasa inakumbwa na mawimbi makali na mazingira hatarishi, jambo linalowaogopesha watalii na kuwazuia kufika kwenye maeneo ya ufukweni.
Hata hivyo, wameeleza kuwa wana matumaini kuwa hali hiyo ni ya muda na biashara zao zitaimarika pindi hali ya hewa itakaporejea kuwa ya kawaida.
Business
Wito kwa Wanawake Wafanyabiashara Jijini Mombasa Kuungana na Kukuza Masoko Yao

Wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo katika jiji la Mombasa wametakiwa kuungana kupitia vikundi ili kuimarisha masoko ya bidhaa na huduma zao, si tu ndani ya nchi bali pia kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Collaboration of Women in Development (CWID), Bi. Betty Sharon, amesema kuwa licha ya juhudi kubwa zinazowekwa na wanawake katika sekta ya biashara ndogondogo, bado wanakumbwa na changamoto nyingi zinazokwamisha mafanikio yao.
Bi. Sharon amesisitiza haja ya kuwajengea uwezo wanawake hao kupitia mafunzo ya kibiashara na kuwawezesha kupata raslimali muhimu kama mitaji, teknolojia, na taarifa za masoko, ili kuongeza viwango vya uzalishaji na kuvuka mipaka ya soko la ndani.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake wafanyabiashara wakiongozwa na Bi. Beatrice Simiyu, wameitaka serikali pamoja na wahisani kuongeza juhudi katika kuwawezesha kwa kuwapatia ujuzi wa kibiashara na miundombinu bora ya kufanikisha biashara zao.