News
Wahudumu wa Tuktuk Malindi washinikiza uhamisho wa Trafiki.

Wahudumu wa sekta ya Tuktuk mjini Malindi kaunti ya Kilifi wamelalamika kuhangaishwa na maafisa wa trafiki mjini humo licha ya kutimiza vigezo hitajika vya kuwaruhusu kuhudumu barabarani.
Mwenyekiti wa wahudumu hao kaunti ya Kilifi Abdhalla Mwangi alisema kuwa serikali inafaa kukifanyia mabadiliko kitengo hicho ili kutatua mzozo uliopo baina ya wahudumu hao na maafisa wa trafiki.
Mwangi alisistiza haja ya swala hilo kuangaziwa kwa kina kutokana na kile alichodai kuwa hali hiyo imeathiri pakubwa sekta hiyo kiuchumi.
“Hawa trafiki hawaturidishi kabisa, Malindi ulikuwa ni mji mzuri ambao unautulivu saa hii unaweza kubebwa na dereva, atazunguka kitambo afike mahali anaenda yaani hata wewe mwenyewe utamuonea huruma, hawa jamaa wamekuwa niusumbufu saa hii sio oparesheni”, alisema Mwangi.
.
Maafisa wa trafiki katika barabara za humu nchini(picha kwa hisani)
Mwangi aidha alibainisha kuwa licha ya kuwasilisha ombi la kutaka uhamisho wa maafisa wa trafiki waliohudumu kwa muda mrefu mjini humo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na serikali kufikia sasa
“Nilizungumza na serikali kuwaomba kwamba kuna maafisa wa trafiki hapa kwetu ambao hawana nidhamu za kikazi na wanagonganisha madereva na serikali, tukaomba serikali hawa watu wahamishwe, na mpaka sasa hatujaona hatua yeyote ambayo imefanyika”,aliongeza Mwangi
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi