Business
Wafugaji wa Nyuki Lamu Walia Kudorora kwa Biashara ya Asali Kutokana na Asali Ghushi

Wafugaji wa nyuki katika Kaunti ya Lamu wamelalamikia kuporomoka kwa soko la asali halisi, wakilaumu kuongezeka kwa asali ghushi inayojaa sokoni.
Kwa mujibu wa wafugaji hao, baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakichanganya sukari kwenye asali na kuiuza kwa bei ya chini, hali inayovuruga ushindani wa haki na kuharibu sifa ya bidhaa ya asali asilia.
Wakizungumza na vyombo vya habari, walisema kuwa biashara yao sasa inaendelea kusambaratika huku wateja wakipungua kwa kasi, wakihofia kununua bidhaa zisizo halisi. Wamekadiria hasara kubwa na kupoteza wateja waliokuwa wa kudumu.
Katika hatua ya kukabiliana na tatizo hilo, mamlaka husika zimeonya kuwa wafanyabiashara wanaouza asali ghushi watachukuliwa hatua kali za kisheria. Wametakiwa kusitisha mara moja biashara hiyo haramu inayowahujumu wakulima halali.
Aidha, wito umetolewa kwa wanunuzi kuwa waangalifu wanaponunua asali, kuhakikisha wanachukua bidhaa kutoka kwa vyanzo vinavyoaminika ili kuepuka kununua bidhaa bandia.
Business
Vijana Kaunti ya Tana River Waanzisha Biashara ya Sambusa za Samaki kuinua Uchumi

Vijana katika Kaunti ya Tana River wameanzisha biashara ya upishi wa sambusa za samaki kwa lengo la kujikwamua kiuchumi kwa kutumia rasilimali za baharini.
Wamebuni mbinu ya kipekee ya kuandaa sambusa kwa kutumia samaki wa aina mbalimbali, wakiwemo samaki papa. Mbali na sambusa, vijana hao pia wameweza kuunda bidhaa nyingine za thamani kutokana na samaki, hatua inayochochea ubunifu na kuongeza ajira miongoni mwao.
Kulingana na vijana hao, biashara hiyo inalenga kuongeza kipato chao na kufungua milango ya kuingia katika masoko mapya, ya ndani na hata ya nje ya kaunti.
Hatua hii imesukumwa na changamoto ya uhaba wa soko la samaki katika eneo hilo, hali ambayo husababisha uharibifu wa samaki kutokana na kukosa wanunuzi. Kwa hivyo, ubunifu huu umekuwa suluhisho la kiuchumi na kiteknolojia kwa vijana wa Tana River.
Business
Wafanyabiashara wa Soko la Matano Mane Waililia Serikali ya Kaunti ya Kilifi Kuwajengea Choo

Wafanyabiashara katika soko la Matano Mane, eneo la Vitengeni, Kaunti ya Kilifi, wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuwajengea choo, wakisema ukosefu wa huduma hiyo muhimu umekuwa kero kubwa inayozorotesha shughuli za biashara.
Wakiongozwa na Phelisia Mageshi, wafanyabiashara hao wamesema kuwa hali ya sasa imesababisha baadhi yao kuhamishia biashara zao nje ya soko hilo, kutokana na mazingira yasiyofaa kwa shughuli za kila siku.
Bi Mageshi ameeleza kuwa licha ya serikali ya kaunti kufahamishwa kuhusu changamoto hiyo mara kadhaa, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa, hali inayowafanya kuhisi kusahaulika.
Wameitaka serikali ya kaunti kuingilia kati kwa haraka ili kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na kuhakikisha afya ya wananchi inalindwa.