News
Duale, asitisha huduma za vituo vya afya 40 kwa udanganyifu wa SHA

Waziri wa afya nchini Aden Duale amethibitisha kusitishwa kwa shughuli za vituo 40 vya afya ambavyo vilibainika kujihusisha na udanganyifu dhidi ya mamlaka ya bima ya afya ya SHA.
Akizungumza jijini Nairobi, Duale alisema usitishaji huo umeanza kutekelezwa mara moja na katika kipindi cha uchunguzi vituo hivyo havitapokea fedha zozote kutoka kwa SHA na vitawajibishwa kwa kurejesha fedha zilizopotea.
Vilevile, wizara hiyo iliwatambua wahudumu kadhaa wa afya ambao walihusika katika ufisadi na ubadhirifu wa raslimali za serikali wakiwemo madaktari 8 kutoka maeneo ya Bungoma, Nairobi na Kilifi.
Wizara ya afya haitaruhusu visa kama hivyo kuendelezwa kwenye vituo vya afya nchini na watakabiliwa kisheria’’ Alisema Duale
Duale pia alisema mikakti thabiti imewekwa kuhakikisha sekta ya afya nchini inaimarishwa vilivyo.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.