News
Viongozi wa upinzani waendelea kuisuta serikali

Viongozi wa upinzani wameikosoa serikali kwa kukosa kutekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi hasa katika kufufua miradi ya kiuchumi nchini.
Wakiungumza katika kaunti ya Kakamega viongozi hao wakiongozwa na kinara wa Chama cha DCP Rigathi Gachagua waliomba wakaazi kushirikiana na kuiondoa serikali katika uchaguzi mkuu ujao.
Viongozi hao walimshtumu Rais William Ruto pamoja na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kile walichosema ni kuwatelekeza wakaazi wa ukanda wa magharibi kila msimu wa baada ya uchaguzi mkuu.
“Nyinyi mnampatia kura anatoa fujo, anaitwa, anaingia kwa serikali anawaacha nyinyi kwa mataa, sasa mimi nimefukuza Ruto kule kwa mlima, nimefunga mlima kifunguo iko hapa kwa gari”,alisema Gachagua.
Kwa upande wake kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alieleza matumaini ya ushirikiano wao na Gachagua, akisema wanaamini wakipata uungwaji mkono wa wananchi wanambandua rais Ruto mamlakani.
Viongozi hao wanasema serikali imeshindwa kudhibiti taifa hasa kupunguza gharama ya maisha na kutimiza ahadi ya miradi ya maendeleo ya kufaidi mahasla.
“Sisi tumekosana na William Ruto kwa sababu ule mkataba ambao tuliandishana naye kama watui wa mkoa wa magharibi amekataa”,alisema Cleophas Malala.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi