News
Viongozi wa kisiasa wampigia debe Joho kuwa Kiongozi wa Pwani

Baadhi ya viongozi wa kisiasa kaunti ya Mombasa wanaendelea kumpigia debe Waziri wa madini na uchumi wa bahari na maziwa nchini, Ali Hassan Joho kuwa Kiongozi wa Pwani, ambaye atapeperusha bendera ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2032.
Viongozi hao wakiongozwa na Mwakilishi wa kike kaunti ya Mombasa Zamzam Mohamed wamesema Waziri Joho ana uwezo mkubwa wa kuliunganisha eneo la Pwani ili liweze kunufaika kimaendeleo kama maeneo mengine nchini.
“Leo rais ametutunuku, ametupatia Hassan Ali Joho kama Waziri wa Blue Economy ambayo inahusu kaunti zetu, na Waziri Hassan Joho anachapa kazi, kwa hivyo safari yetu sisi tumeianza’’, alisema Zamzam.
Zamzam alisema Joho amekuwa kwenye siasa kwa miaka mingi na ana uzoefu katika uongozi, hivyo basi anapaswa kupeperusha bendera hiyo.
Ni kauli ambayo imeunga mkono na Mbunge wa Jomvu Badi Twalib ambaye amesisitiza ushirikiano baina ya viongozi ili kuhakikisha malengo hayo yanaafikiwa ipasavyo.
Naye Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba alisema maeneo mengine ya nchi yanajiandaa kuwa na kiongozi ambaye ataliongoza taifa hili na kusisitiza umuhimu wa Wapwani kushirikiana ili Joho aweze kuwa rais wa taifa hili mwaka wa 2032.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
IEBC inaendelea kutambua vituo vya kusajili wapiga kura

Maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wamesema wanaendelea na zoezi la kutambua sehemu za kuweka vituo vya kusajili wapiga kura hasa maeneo ya mashinani.
Afisa msimamizi wa tume ya IEBC eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi, Mohammed Bahero Aboud alisema juhudi hizo ni kuhakikisha zoezi la usajili wapiga kura litakaloanza rasmi Septemba 29, mwaka huu linafaulu.
Akizungumza mjini Kilifi, Bahero alisema tume hiyo inatumia mbinu mpya ya kutambua vituo vya jadi vya usajili wapiga kura na kuweka vituo vipya kulingana na mapendekezo ya sheria.
Wakati huo huo alidokeza kwamba tume ya IEBC imekuwa ikihamashisha wakenya kutokubali kushawishiwa na wanasiasa na kujisajili katika maeneo yasiokuwa yao hasa msimu huu ambao zoezi hilo linakaribia kuanza.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Kaunti ya Mombasa kukumbatia matumizi ya mfumo wa miale ya jua

Serikali ya kaunti ya Mombasa imesema imeanza kutekeleza mpango wa kutumia nishati mbadala katika vituo vyote vya huduma za kaunti, kwa kuanza na mabadiliko ya mfumo wa taa hadi kutumia umeme wa miale ya jua.
Kwa mujibu wa waziri wa kawi, rasilimali asili na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kaunti ya Mombasa, Emily Achieng, hatua hii inalenga kupunguza gharama za matumizi ya umeme na kuhimiza matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Mbali na hilo, waziri huyo alisema kaunti inaendelea kuweka vifaa maalum vya kupima ubora wa hewa katika maeneo mbalimbali ya mji na ndani ya taasisi za umma.
Lengo ni kupata ushahidi wa kisayansi kuhusu kiwango cha uchafuzi wa hewa, na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wanaokiuka sheria.
Vifaa hivyo tayari vimewekwa katika hospitali ya rufaa ya Coast General na baadhi ya shule ikiwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kaunti, kujenga ustahimilivu dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Mikakati hiyo pia itasaidia kaunti katika kufanya maamuzi kuhusu maeneo yanayofaa kuwekwa biashara fulani, ili kulinda wananchi dhidi ya maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.