News
Vijana waitaka serikali kuzingatia sheria

Vijana na wanaharakati wa maswala ya vijana kaunti ya Mombasa wanaitaka serikali ya kitaifa kutekeleza maswala ya msingi yanayohusu uongozi na utawala wa sasa.
Vijana hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Nyali Youth Association Evans Mtalii walisisitiza kuwa hawataki mazungumzo bali hatua za msingi kufanyika.
Mtalii alisema serikali imekuwa ikipuuza kilio na changamoto wanazopitia vijana ikiwemo utekaji nyara, mauwaji ya kiholela na ukiukaji wa haki za kibinadamu miongoni mwa changamoto zingine.
“Hatuhitaji mazungumzo kukomesha utekaji nyara, kukomsha mauwaji ya kiholela sisi tushawaambia matatizo na changamoto ambazo tunataka serikali iangazie hivyo sio lazima watuite kwa mazungumzo rekebisheni peke yenu bila ya kutuita kwa mazungumzo”. … alisema Evans
Mtalii vile vile alisema inasikitisha kuona kwamba kuna baadhi ya viongozi wanaoyafumbia macho madhila wanayopitia vijana.
Wakati huo huo Edwin Shamiri alimsihi rais William Ruto kuhakikisha kuwa anaongoza nchi kulingana na katiba.
Shammir alisema wapo tayari kama wakereketwa kutete na kuhakikisha haki za mwananchi hazikiukwi kivyovyote vile.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi