Business
Tezo: Wakulima Watarajia Mavuno Tele ya Mahindi

Wakulima wa mahindi humu nchini wanasema kuwa wanatarajia mavuno bora mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.
Kulingana na wakulima hao mvua inayoendelea kunyesha kote nchini inawapa matumaini kupata mavuno mengi mno ikilinganishwa na msimu uliopita.
Wakizungumza na cocofm wakulima hao kutoka eneo la Tezo kaunti ya kilifi wamesema kuwa bei ya mahindi inatarajiwa kuteremka kwani mahindi yatakuwa yanapatikana kwa wingi hali ambayo itawapa wananchi afueni.
Hata hivyo wameitaka serikali kuweka mikakati ya kununua mahindi kutoka kwao na kwa bei nzuri ili kuwainua kiuchumi.
Business
Kanda ya Pwani kuimarika kupitia Kilimo cha kisasa

Kanda ya Pwani inatarajiwa kuimarika zaidi kupitia Kilimo cha kisasa kinachotekelezwa kupitia mfumo wa teknolojia.
Hii ni kupitia mikakati inayoendelezwa na Agitech Seedlings kuhakikisha Wakulima na Wenyeji wa Kanda ya Pwani wanakumbatia Kilimo cha kisasa kama maeneo mengine nchini.
Akizungumza na Coco FM katika maonyesho ya Kilimo cha kisasa na uzinduzi wa tawi jipya la Agitech Seedling katika eneo la Kwa Ndomo mjini Malindi kaunti ya Kilifi, Mkurugenzi wa Agitech Seedlings Peter Karanja Ndung’u alieleza sababu za kuanzisha Kilimo hicho cha kisasa katika ukanda wa Pwani.
Karanja pia alisema wanapania kuhakikisha wenyeji wa Pwani wanahamasishwa ipasavyo na hata kuonyeshwa namna ya kufanya Kilimo hicho hapa pwani.
“Kupitia hamasa ambazo tunatoa kwa wakulima na wenyeji wa Pwani kwa jumla tunatarajia kuwa Kilimo kitaanza kuimarika na kuondoa dhana ambayo imekuwepo kwamba eneo la Pwani linatambulika pekee kwa masuala ya uvuvi’’, alisema Karanja.
Vilevile, Karanja alisema kuna haja ya Wakulima kutunza ardhi zao kwa kuhakikisha zina rutuba ya kutosha ili kuzalisha chakula kwa wingi na bora.
Taarifa ya Janet Mumbi
Business
Wahudumu wa Uchukuzi Kilifi Walia na Kupanda kwa Bei ya Mafuta

Siku moja baada ya mamlaka ya udhibiti wa kawi nchini, EPPRA kutangaza kupandishwa kwa bei ya mafuta, sekta ya uchukuzi katika kaunti ya Kilifi inaelezea hofu ya kuathirika kwa biashara zao.
Wahudumu wa tuktuk,teksi, bodaboda na magari ya usafiri wa umma hapa mjini Kilifi wanasema kupanda kwa bei ya petrol na diseli kutaathiri pakubwa sekta hiyo ya uchukuzi.
Sasa wanasema kuwa watalazimika kuongeza nauli kwa abiria kutokana na gharama ya mafuta.
Ni hali ambayo imeathiri wakaazi ambao wanatarajiwa kutumia vyombo hivyo vya usafiri wakisema kuwa watalazimika kutembea kwa mguu kwa safari fupi fupi katika utekelezaji wa shughuli zao za kawaida.
Hatahivyo wametoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa inaingilia kati ili kuona kwamba bei za mafuta zinadhibitiwa.
Haya yamejiri huku lita moja ya mafuta aina ya petrol kaunti ya KIlifi ikiuzwa kwa shilingi 183.88 huku diseli ikiuzwa kwa shilingi 169.16 kila lita.
Lita moja ya mafuta ya taa inauzwa kwa shilingi 153.29.