News
Rais Ruto aahidi kusaidia sekta ya Boda Boda

Rais William Ruto amesema atawasilisha bungeni pendekezo la kupunguzwa kwa ushuru wa pikipiki ili kuwawezesha vijana kote nchini kuwa na uwezo wa kumiliki pikipiki na kujiimarisha kiuchumi.
Rais Ruto alisema japo kwa sasa bei ya pikipiki hizo imeshuka, jukumu la serikali ni kuhakikisha vijana wanakuwa na uwezo wa kujiimarisha kiuchumi na hatua hiyo itaafikiwa kwa kupunguzwa kwa ushuru wa pikipiki.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi baada ya kukutana na viongozi wa wahudumu wa bodaboda kote nchini, rais Ruto alisema mpango huo utahakikisha mwananchi wa kawaida anamiliki pikipiki kwa kulipia kiwango cha chini zaidi cha shilingi 9,500.
Kiongozi wa nchi, aliwarai vijana kukumbatia mpango huo kwani nia yake ni kuwawezesha vijana kuzikabili changamoto mbalimbali za kimaisha sawa na kudhibiti uchumi wa taifa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi.
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.