News
Prof Kindiki: Uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027 utakuwa huru, haki na amani

Naibu Rais Prof Kithure Kindiki amewahakikishia wakenya kwamba uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2027 utakuwa huru, haki na amani.
Kindiki amemshtumu Kinara wa Chama cha Democracy for the Citizen’s Party {DCP} Rigathi Gachagua, akisema kauli alizozitoa kuhusu uchaguzi mkuu ujao zinalenga kuligawanya taifa kwa msingi ya vurugu.
Kindiki amewataka wakenya kuwa makini na viongozi wasio na ajenda ya maendeleo kwa wananchi na badala yake kushirikiana na serikali ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa mashinani.
Wakati huo huo amewahakikishia wakenya kwamba serikali ya Kenya kwanza iko mbioni kuhakikisha inakabiliana na changamoto za gharama ya maisha, akiwataka wapinzani kuipa nafasi serikali kuwajibikia majukumu yake.
News
Mwanaharakati Mwabili Mwagodi apatikana

Mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Mwabili Mwagodi ambaye alidaiwa kutekwa nyara akiwa nchini Tanzania sasa amepatikana.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za kibinamu nchini la VOCAL Africa Hussein Khalid, alisema Mwabili alipatikana katika msitu wa Kinondo eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale mwendo wa saa tisa usiku akitembea kuelekea Diani.
Khalid alisema Mwabili, anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya mjini Mombasa kisha baadaye atasafirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi kuungana na familia yake.
“Tunashukuru Mwabili amepatikana akiwa hai japo amedhohofika na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Pandya na kisha atarudi Nairobi kukutana na familia yake lakini tunaiambia serikali ya Kenya na Tanzania ni lazima wahusika kukomesha tabia hii ya kuwateka watu nyara kuna sheria kama mtu amekosea apelekwe Mahakamani”, alisema Khalid.
Hata hivyo Wanaharakati hao wa kutetea haki za kibinadamu waliishtumu serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwanyanyasa wanaharakati wa kijamii wa taifa la Tanzania na wale wanaoingia Tanzania kutoka mataifa mengine ili kuendeleza hamasa za haki za kijamii.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Herman yahairishwa

Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara ambaye ni raia wa Uholanzi, Rowenhorst Herman na mlinzi wake Evans Bokoro imeahirishwa hadi mwezi Oktoba mwaka huu kufuatia Mahakama kuingia kwenye mapumziko rasmi ya majaji.
Mke wa Marehemu, Riziki Cherono pamoja na mshukiwa mwenza Timothy Omondi wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga na kutekeleza mauaji hayo yaliyotokea Juni 4 mwaka 2021 katika eneo la Shanzu kaunti ya Mombasa.
Katika kikao cha awali cha Mahakama, Afisa wa Polisi Koplo Richard Cheruiyot alieleza mbele ya Jaji Wendy Micheni kwamba Cherono alijaribu kuonekana kama mwathirika kwa madai ya kutekwa nyara na majambazi waliodaiwa kuvamia nyumba yao.
Afisa huyo alieleza kwamba walimkuta Cherono akiwa amefungwa kwenye usukani wa gari lake, huku akidai kwamba alivamiwa na kulazimishwa kuondoka nyumbani kwao akiwa chini ya tishio la bunduki.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa ulibaini kwamba Marehemu Herman alipatikana amefariki nyumbani kwake akiwa amefungwa mikono na miguu huku mlinzi wao, Evans Bokoro, alikutwa akiwa hai kwa taabu karibu na bwawa la kuogelea lakini baadaye alifariki akipelekwa hospitalini.
Mashahidi wa upande wa mashtaka pamoja na polisi, wanaamini kwamba Cherono ndiye mshukiwa mkuu wakidai kwamba alipanga na kufanikisha mauaji hayo kwa kushirikiana na watu wengine, wakiwemo waliotajwa kuwa sehemu ya genge lililovamia nyumba hiyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
Baba Yaga
May 19, 2025 at 9:44 pm
Hii Imeenda