Serikali imewaonya wakenya hasa Vijana wa Gen Z kutokubali kushurutishwa na Wanasiasa na kushiriki maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura, aliwataka vijana kutokubali kushiriki maandamano ya siku ya Jumanne Aprili 21, akisema yatachangia kuharibika zaidi kwa uchumi wa taifa.
Katika kikao na Wanahabari jijini Nairobi, Mwaura alisema maandamano sio suluhu la kutatua changamoto zinazoshuhudiwa nchini bali yatachangia hasara kwa taifa ambalo linakuwa kiuchumi na maendeleo, akisisitiza haja ya wakenya kutafuta njia mbadala za kuwasilisha lalama zao na wala sio kushiriki maandamano.
Mwaura alisema maandamano yaliofanyika mwezi Juni mwaka 2024, yalichangia taifa kupata hasara ya shilingi bilioni 6, kulingana na takwimu za Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, akiwataka wakenya kujitenga na maandamano hayo.
“Maandamano ya Juni mwaka wa 2024, alisababisha taifa kupata harasa ya zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa hivyo haitakuwa bora kwa wanasiasa kuwatumia vijana vibaya kuharibu mali ya umma, hivyo basi wanasiasa wafanye mipango ya kuwatafutia kazi vijana”, alisema Mwaura.
Maandamano hayo yanalenga kuishinikiza serikali kupunguza bei ya mafuta nchini licha ya taifa kukumbwa na msukosuko wa changamoto za mafuta yaliochangiwa na sakata ya ufisadi ya uagizaji mafuta pamoja na mgogoro wa vita nchini Iran.
Vijana wa kizazi cha Gen Z, wamekuwa wakiikosoa serikali kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, tangu mwaka wa 2024 huku maandamano ya mara kwa mara nchini yakishuhudiwa katika baadhi ya maeneo, wakenya wakilalamikia kunyanyaswa na serikali.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
