Mamlaka ya usafiri wa majini nchini (KMA), imethibitisha kupokea taarifa kuhusu kuzuiliwa kwa meli yenye bendera ya Kenya katika nchi ya Tanzania.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, KMA imesema meli hiyo inayojulikana kama MV SEA MFALME kwa sasa inashikiliwa nchini humo.
Maafisa wa Mamlaka hiyo, wale wa ujasusi, na wanajeshi wa majini wameanzisha uchunguzi kubaini sababu za tukio hilo, na kama meli hiyo ilikuwa imebega shehena gani ndiposa ikazuiliwa.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa inashirikiana kwa karibu na mashirika ya kiserikali pamoja na wadau katika nchi zote mbili ili kubaini kilichosababisha kuzuiliwa kwa meli hiyo na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa.
Mamlaka hiyo ilielezwa kwamba tayari imeijulisha Wizara ya masuala ya kigeni nchini inayoongozwa na Waziri Musalia Mudavadi ili kusaidia katika masuala ya kidiplomasia kwani hatua hiyo huenda ikachangia sintofahamu za kimataifa.
KMA imewahakikishia wadau wa sekta hiyo na wamiliki wa meli hiyo kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa kufuata taratibu za kisheria na ushirikiano wa kimataifa, na kwamba taarifa zaidi zitatolewa kadri uchunguzi unavyoendelea.
“Tunashirikiana na wadau mbalimbali kwa kuzingatia sheria za kimataifa na ushirikiano wa kidiplomasia kuhusu suala hilo na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa”, alieleza afisa mmoja wa Mamlaka hiyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
