IEBC yapiga marufuku matumizi ya simu kwenye vituo vya upigaji kura

IEBC yapiga marufuku matumizi ya simu kwenye vituo vya upigaji kura

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, imepiga marufuku matumizi ya simu za rununu kwenye eneo maalum la upigaji kura wakati wa zoezi la uchaguzi.

Kamishna wa Tume ya IEBC, Alutalala Mukhwana amesema tume hiyo imechukua uamuzi huo ili kuhakikisha kuna kuwepo na usiri wa upigaji kura.

Alutalala alisema katika chaguzi za hivi karibuni, baadhi ya wakenya walionekana kutumia simu zao za rununi kupiga picha kwenye eneo maalum la upigaji kura katika baadhi ya vituo vya kupiga kura.

Akizungumza baada ya kufungua rasmi zoezi la upigaji kura katika eneo bunge la Isiolo kusini, Alutalala alisema tabia hiyo haitaruhusiwa tena kwani ni ukiukaji wa Katiba na sheria za uchaguzi za nchi.

Kwa upande wake, Msimamizi wa uchaguzi katika eneo bunge la Isiolo kusini Abdi Sheikh alisema maafisa wa IEBC wamejiandaa vyema kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na haki.

Wakati huo huo Afisa mkuu wa polisi eneo la Garbatulla Pius Mbithi, aliwahakikisha wakaazi wa eneo bunge hilo linaloandaa uchaguzi mdogo, usalama wa kutosha.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi