News
Mwili na mafuvu mawili yapatikana karibu na Shakahola

Maafisa wa polisi kaunti ya Kilifi wamewaokoa watu wanne katika kijiji cha kwa Binzaro kilomita 6 kutoka Shakahola.
Kamishna wa kaunti ya Kilifi Josephat Biwot alisema oparesheni hiyo iliyohusisha wakaazi, watu watatu kati ya wanne waliookolewa wameonekana wakiwa dhaifu kuliko hali yao ya kawaida.
Mwili mmoja na mafuvu mawili ya binadam pia yamepatikana nyumbani humo.
Biwot alidokeza kuwa wahusika hawakupatikana nyumbani wakati wa oparesheni hiyo na haijabainika kilichokuwa kikiendelea.
Mwili na mafuvu hayo yalipelekwa katika hifadhi ya maiti ya katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Boniface Mwangi akamatwa na maafisa wa DCI

Mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu nchini Boniface Mwangi amekamatwa na maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI.
Kulingana na Mkewe Boniface, Hellen Njeri Mwangi, Mumewe amekamatwa nyumbani wako katika eneo la Lukenya kaunti ya Machokos na maafisa waliojitambulisha kwamba wanatoka katika Idara ya DCI.
Hellen alisema Boniface amepelekwa katika makao makuu ya idara ya DCI jijini Nairobi huku sababu za kukamatwa kwa Boniface zikihusisha na masuala ya ugaidi.
Kulingana na Wakili wa Boniface, James Kamau alisema maafisa wa DCI walivamia makaazi ya mteja wake wakiwa wamejihami kwa silaha na kumtia nguvuni.
Hatua hii imejiri baada ya Boniface na Mwanaharakati kutoka Uganda Agather Utuhaire mnamo siku ya Ijumaa Julai 18, 2025 kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki na kulishtaki taifa la Tanzania kwa madai kwamba maafisa wa serikali ya Tanzania walikiuka haki zao za kibinadamu.
Kwenye mashtaka hayo, Wanaharakati hao walidai kutekwa nyara na watu wasiojulikana wakiwa jijini Dar er Salam pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na kutupwa nje ya mpaka wa Tanzania, Uganda na Kenya, mtawalia.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Ethekon: Tutaandaa uchaguzi huru na haki, 2027

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imewahakikishia wakenya kwamba itafanikisha uchaguzi huru na haki ifikapo mwaka wa 2027.
Kulingana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Erastus Ethekon, IEBC iko tayari kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, ikiwemo usajili wa wapiga kura, kuendesha uchaguzi, pamoja na kugawaa mipaka ya maeneo ya uwakilishi.
Akizungumza mjini Mombasa tangu kuapishwa kwake kushikilia wadhfa ya Mwenyekiti wa IEBC, Ethekon alisema IEBC itaharakisha mchakato wa kuandaa chaguzi ndogo 23 kote nchini ikiwemo nafasi moja ya Seneta, nafasi 6 za ubunge na nafasi 16 za uwakilishi wadi.
Ethekon alisema nafasi hizo za viongozi ziliachwa wazi baada ya baadhi ya viongozi kupoteza maisha yao huku wengine viti vya vikasalia wazi baada ya matokeo ya chaguzi hizo kubatilishwa na Mahakama.
Wakati huo huo aliwataka wanasiasa kujiepusha na matamshi yanayoashiria uwepo wa njama za wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao, akisema kauli hizo zinatia doa utendakazi wa tume ya IEBC huku akilitaka bunge la kitaifa pamoja na Wizara ya Fedha nchini kuhakikisha tume hiyo inapokea mgao wa fedha kwa wakati.
Ethekon alisisitiza kuwa tume hiyo iko imara na haitashuhudia migawanyiko kama ilivyoshuhudiwa katika vipindi vilivyopita.
Taarifa ya Mwanahabari wetu