News
Mwaura: Hakuna Mswada wa Fedha wa Mwaka 2025 uliyowasilishwa Bungeni

Serikali imejitokeza na kupinga taarifa zinazoendelea katika mitandao ya kijamii kwamba inalenga kuwasilisha mswada wa fedha wa mwaka wa 2025 bungeni ambao unalenga kuongeza ushuru kwa wakenya.
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema taarifa hizo ni propaganda zisizo na ukweli wowote na ambazo zinalenga kuwagonganisha wakenya kama ilivyoshuhudiwa mwezi Juni mwaka wa 2024 wakati wananchi walipozua vurugu kupinga mswada wa fedha.
Katika kikao na Wanahabari katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi, Mwaura amesema japo serikali iko na mipango ya kutengeneza bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026, ni lazima wananchi wahusishwe kikamilifu katika vikao vya kutoa maoni ya umma.
Msemaji huyo wa serikali amebainisha kwamba serikali itahakikisha inawashikiza wakenya wanaokwepa kulipa ushuru kuwajibika huku akisema wakenya zaidi ya milioni 8.5 wamenufaika na bima ya Afya ya Taifa Care.
Wakati huo huo ameelezea hatua zilizopigwa na serikali za kimaendeleo katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa, akisisitiza haja ya wakenya kuunga mkono serikali kufanikisha ajenda yake ya maendeleo kwa wananchi wote.
News
Joho atangaza kuwania urais siku zijazo

Waziri wa madini na masuala ya bahari nchini Hassan Ali Joho, alidokeza kwamba katika siku zijazo eneo la Pwani litatoa rais wa taifa la Kenya.
Waziri Joho aliwataka wakaazi wa Pwani kutojiingiza katika mivutano ya kisiasa na mirengo mingine ya kisiasa nchini, akisema ni wakati mwafaka wa wapwani kuungana na kujipanga kisiasa.
Waziri Joho alisema mtu ambaye alikuwa na nafasi nzuri ya kushikilia wadhfa huo wa kitaifa aliyekuwa ni Marehemu Karisa Maitha lakini ndoto hiyo bado ipo, akiweka wazi kwamba anamezea mate kiti hicho katika siku zijazo.
“Mara ya kwanza nilifikia kama kuna mpwani anaweza kuwa rais ilikuwa ni marehemu Karisa, lakini mimi hiyo ndoto bado niko nayo na nina imani iko siku bado hapa Pwani kuzaa rais. Siku moja wataskia rais Hassan na nikujipanga”, alisema Joho.
Joho alisisitiza haja ya wapwani kujipanga kisiasa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kuvuna kwenye ngazi ya kitaifa pamoja na kuwa rahisi kwa eneo la Pwani kuwania kiti hicho na kutangaza rais wa Kenya katika siku zijazo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Waziri Joho na Mvurya waonya wanyakuzi wa ardhi.

Waziri wa madini na uchumi wa bahari nchini Ali Hassan Joho alisema serikali haitaruhusu tena wakaazi kufurushwa katika ardhi wanayoishi.
Akizungumza katika maeneo ya Mzambarauni mjini Mtwapa eneo bunge la Kilifi Kusini kaunti ya Kilifi, Joho alionya kwamba mabwenyenye wenye hulka ya kufurusha wananchi kwenye ardhi za umma kamwe hawataruhusiwa.
Joho alisema wananchi hawafai kuhangaishwa kwenye ardhi zao huku akiwatahadharisha maafisa wa serikali dhidi ya kushirikiana na mabwenyenye kuhangaisha raia kwenye ardhi zao.
Hii ni baada ya kuibuka malalamishi ya mabwenyenye kutaka kuwafurusha wakaazi wa Utange Kaunti ya Mombasa.
Kwa upande wake Waziri wa michezo na Sanaa nchini Salim Mvurya alidokeza kuwa serikali inapanga kununua mashamba ambayo hayatumiki ili kuyakabidhi ya wananchi.
Taarifa ya Joseph Jira