News
Mwaura: Hakuna Mswada wa Fedha wa Mwaka 2025 uliyowasilishwa Bungeni

Serikali imejitokeza na kupinga taarifa zinazoendelea katika mitandao ya kijamii kwamba inalenga kuwasilisha mswada wa fedha wa mwaka wa 2025 bungeni ambao unalenga kuongeza ushuru kwa wakenya.
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema taarifa hizo ni propaganda zisizo na ukweli wowote na ambazo zinalenga kuwagonganisha wakenya kama ilivyoshuhudiwa mwezi Juni mwaka wa 2024 wakati wananchi walipozua vurugu kupinga mswada wa fedha.
Katika kikao na Wanahabari katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi, Mwaura amesema japo serikali iko na mipango ya kutengeneza bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026, ni lazima wananchi wahusishwe kikamilifu katika vikao vya kutoa maoni ya umma.
Msemaji huyo wa serikali amebainisha kwamba serikali itahakikisha inawashikiza wakenya wanaokwepa kulipa ushuru kuwajibika huku akisema wakenya zaidi ya milioni 8.5 wamenufaika na bima ya Afya ya Taifa Care.
Wakati huo huo ameelezea hatua zilizopigwa na serikali za kimaendeleo katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa, akisisitiza haja ya wakenya kuunga mkono serikali kufanikisha ajenda yake ya maendeleo kwa wananchi wote.
News
Maandalizi ya Maadhimisho ya Chenda Chenda

Ni dhahiri sasa kutakuwa maaadhimisho ya Chenda Chenda siku ya Jumanne Septemba 9, 2025 kwa wakati mmoja katika kaunti ya Kwale na kaunti ya Kilifi.
Waasisi wa maadhimisho haya ambao ni wWazee wa kutoka Kaya zote za Wamijikenda walitangaza mwaka uliopita kwamba maadhimisho ya mwaka huu yafanyika katika kaunti ya Kwale baada ya kuandaliwa eneo la Kaya fungo kaunti ya Kilifi mwaka jana.
Na baada ya vikao vya mashauriano baina ya Wazee wa Kaya zote hivi majuzi katika eneo la Rabai, Wazee hao waliafikiana kwa kauli moja kwamba maadhimisho hayo ya mwaka huu yaandaliwe katika Kaya ya Mtswakara eneo bunge la Kinango katika Kaunti ya Kwale.
Lakini baada ya tangazo hilo kutolewa, serikali ya kaunti ya Kilifi ilitangaza kufanya maadhimisho hayo katika uwanja wa chuo kikuu cha Pwani.
Tangazo hilo liliwaghadhabisha mno Wazee wa Kaya ambao katika taarifa kwa Wanahabari walisema wanaendelea na mipango ya maadhimisho hayo katika kaunti ya Kwale.

Maandalizi ya Maadhimisho ya Chenda Chenda, kaunti ya Kilifi
Hali hii imezua tofauti kubwa baina ya Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Mung’aro anayedaiwa kuenda kinyume na utaratibu wa tamaduni za Kaya, ambapo maadhimisho hayo yanapasa kufanyika katika viwanja vya Kaya kama njia moja ya kuwaheshimu wavyele wa Kaya za Kimijikenda.
Huku hayo yakijiri maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea katika uwanja wa Chuo kikuu cha Pwani.
Wazee wa Kaya wanalaumu kitendo hiki na kuongeza kwamba maandalizi haya yanamsukumo wa kisiasa na wala sio ule wa kitamaduni na unaokusudiwa kuleta umoja wa Wamijikenda.
Taarifa ya Eric Ponda
News
Jopo la kushughulikia fidia kwa waathiriwa wa maandamano laanza kazi

Jopo lililoundwa na Rais William Ruto kushughulikia masuala ya fidia ya waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maadamano limeanza kikao cha wiki moja huku mjadala kuhusu uhalali na uwazi wa jopo hili ukitiliwa shaka na kupokea upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu na viongozi wa upinzani.
Jopo hilo linaongozwa na Prof. Makau Mutua na naibu wake Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Faith Odhiambo, ambaye uteuzi wake umeibua mjadala mkali.
Baadhi ya Wanasheria walimshutumu Odhiambo kwa “kusaliti haki,” lakini yeye alisisitiza kwamba jukumu lake ni kuhakikisha waathiriwa wa ukatili wa polisi wanapata haki waliyoikosa kwa muda mrefu.
Aliongeza kuwa jopo hilo lina nafasi ya kuleta mabadiliko ya kihistoria katika upatikanaji wa fidia kwa waathiriwa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, jopo hilo si tume ya kikatiba wala chombo cha kisheria chini ya Katiba, bali ni jopo la ushauri lililoanzishwa na Rais chini ya Kifungu cha 132(4)(a).
Vile vile alibainisha kuwa wanachama wa jopo hilo si maafisa wa umma hivyo uteuzi wao hauhitaji mchakato wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 260 cha Katiba.

Jopo lililoundwa na Rais William Ruto kushughulikia ya fidia ya waathiriwa wa maadamano
Hata hivyo, wakosoaji walisema linaweza kukiuka mamlaka ya ofisi huru kama Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR). Jopo hilo limekanusha madai hayo, likisema jukumu lake ni kusaidia na sio kuchukua nafasi ya taasisi zilizopo.
Wapo pia wanaouliza uhalali wa serikali kuwalipa fidia waathiriwa ilhali serikali hiyo hiyo imeshtumiwa kwa mauaji, kutoweka kwa baadhi ya wakosoaji wa serikali kwa njia tatanishi na kuacha familia na majeraha yasiyotibika.
Jopo hilo pia linasisitiza kikatiba, serikali ndiyo chombo kinachobeba wajibu wa kurekebisha madhila kwa niaba ya taifa. Hata kama madhara yalisababishwa na maafisa wa serikali, haitazuiwa kuwafidia waathiriwa.
Taarifa ya Elizabeth Mwende