News
Mwashako, amtaka Waziri Duale kuwataja wanaohusika na sakata ya SHA

Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako alielezea kukerwa na madai ya ufisadi yanayoendelea kushughudiwa humu nchini hasa kwenye Bima ya afya ya jamii nchini SHA.
Mwashako alisema ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wakijadili suala hilo bila kuchukua hatua zozote mwafaka, hali ambayo inachangia wananchi wengi kutokuwa na imani na viongozi wao.
Mwashako ambaye pia ni Mwenyekiti wa Muungano wa wabunge wa Pwani alimtaka Waziri wa Afya nchini Aden Duale kuwataja hadharani wale wanaohusika na sakata za ufisadi kwenye bima hiyo, akisisitiza kwamba hatua hiyo itasaidia kuimarisha utendakazi wake kama Waziri.
“Kila siku pesa zinapotea, tuseme tu ukweli mimi kama Mwashako inanisumbua sana ndio maana nasema sisi kama viongozi hata mbinguni hatutaenda na siku zote nimekuwa nikimwambia Duale kama uchunguzi imefanywa basi asiogope awataje hadharini wale wetu walihusika na kuiba pesa ya SHA kwa sababu ukiangalia E-Citizen pesa pia inaibwa kila siku”, alisema Mwashako.
Wakati huo huo, alivilaumu vitengo vya usalama nchini hasa Idara ya ujasusi nchini NIS na Idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI kwa kuzembea kuwajibikia majukumu yao huku wananchi wakikabiliwa na madhara kutokana na hali hiyo.
Kauli yake ilijiri huku Kamati ya Afya katika bunge la kitaifa ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni mbunge wa Seme Dkt James Nyikal ikiilaumu Wizara ya Afya nchini kwa kuharibu utekelezaji wa uzidunzi wa Mamlaka ya Afya ya jamiI SHA.
Viongozi wa kamati hiyo walisema changamoto hizo zinaathiri huduma za hospitali mbalimbali za umma nchini sawa na kuwakosesha wagonjwa wengi huduma muhimu za afya.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi

Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi.
Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike alimhukumu Lucky Munga na Hassan Daniel kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya Mahakama kubaini kwamba walihusika kwa kuwatendea unyama watoto wa umri wa miaka 13 na 15.
Safari Karisa Lewa alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kumnajisi mtoto wake mwenyewe wa umri wa miaka 14 huku Eric Ruwa na Lucky Katana Kenga wakihukumiwa kifungo cha miaka 6 gerezani kwa kosa sawa na hilo.
Hata hivyo Mahakama hiyo ilimhukumu kifungo cha miaka 3 Kithi Kombe kutokana na kesi hiyo kwa mtoto wa miaka 15, japo baadaye Mahakama ikabaini kwamba mshukiwa sio baba halali wa mtoto aliyezaliwa baada ya Kithi kumnajisi mtoto huyo.
Akizungumza wakati wa vikao vya Mahakama baada ya kutoa hukumu hizo, Hakimu Wasike alisema Mahakama umezingatia ushahidi uliyotolewa Mahakamani huku akiwarai wananchi kujitenga na visawishi vibaya ili kuepuka mkono wa sheria.
Hakimu Wasike alihoji kwamba washtakiwa wa haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama lakini kwa kuzingatia taratibu zote za Mahakama na sheria.
Taarifa ya Teclar Yeri
News
Thoya: Serikali kuu iongeze mgao wa fedha kwa sekta ya Afya

Naibu gavana wa kaunti ya Mombasa Francis Thoya ametoa changamoto kwa serikali kuu kuongeza mgao wa fedha ili kufanikisha utaoji wa huduma za afya.
Akizungumza katika kaunti hiyo, Thoya alisema kuwa huduma nyingi za afya katika kaunti hiyo ya Mombasa zinakabiliwa na changamoto ya raslimali ndogo hali ambayo inakwamisha juhudi za kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Thoya pia alitaka serikali kuhakikisha inaharakisha kuajiri wahudumu zaidi wa afya ili wenyeji wa Mombasa waweze kupata huduma bora za matibabu bila changamoto zozote.
Aidha, Thoya alisema kwamba hali ya uhaba wa wahudumu wa afya ni changamoto kuu ambayo inazuia utoaji wa huduma bora za matibabu hali inayowafanya wale wachache waliopo kufanya kazi katika mazingira magumu.
Taarifa ya Janet Mumbi