News
Mpango wa Skills Mtaani kufaidi vijana 600 Malindi.

Jumla ya vijana 600 kutoka eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi watanufaika na mpango wa mafunzo ya taaluma za ujuzi, maarufu SKILLS MTAANI unaofadhiliwa na mbunge wa Malindi Amina Mnyazi.
Akizungumza na wanahabari mjini humo, Mnyazi alidokeza kuwa mpango huo utakaotekelezwa kupitia vyuo vya kiufundi vilivyo katika eneo hilo unalenga vijana walio mitaani ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kujistawisha.
Mnyazi alikariri kuwa mpango huo pia utasaidia kupunguza visa vya utovu wa usalama vinavyoshuhudiwa mjini humo kwa kuwapa vijana ujuzi wa kujishughulisha katika jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi kutoka eneo la Kijiwetanga wakiongozwa na Esther Mathias na Katao Nzai Joseph waliupongeza mpango huo wakisema utasaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kupunguza uhalifu katika jamii.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Wakaazi wa Voi waonywa dhidi ya ugonjwa wa MPOX

Daktari wa magonjwa ya kuambukiza katika hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi katika kaunti ya Taita Taveta Urbanius Kioko amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kuzingatia maagizo ya Wizara ya Afya ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Akiongea kwenye warsha ya Wanahabari iliyofadhiliwa na Shirika la Stawisha Pwani, Daktari Kioko alisema wananchi wanapaswa kujikinga ili kudhibiti ugonjwa huo kuenea.
Kioko pia aliwataka wale ambao wana dalili za ugonjwa huo kufika kwenye vituo vya afya ili kutibiwa.
“Huu ugonjwa huwa unaenezwa kupitia kutangamana, kuvaa nguo za mwenzako na kupitia hewa wakati wa kuongea’’, alisema Kioko.

Wadau wa sekta ya Afya katika kikao na Wanahabari mjini Voi
Vilevile, Kioko alitaja kisa cha mgonjwa mmoja wa Mpox kilichothibitishwa siku ya Jumanne wiki hii mjini Voi huku visa vingi vikishamiri katika kaunti Mombasa.
Haya yanajiri huku Wizara ya Afya nchini ikishinikiza wananchi kujiepusha kula nyama za Wanyamapori miongoni mwa tahadhari zingine kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mzozo kati ya Kenye na Tanzania waendelea kutokota

Serikali ya Kenya imeiandikia barua jumuiya ya afrika mashariki kupinga vikwazo vilivyowekwa na Tanzania kuhusu kufanya biashara katika taifa hilo.
Katibu mkuu katika idara ya EAC Daktari Caroline Karugu, alisema kenya imebaini kuwa agizo hilo haliambatani kamwe na masharti muhimu ya itifaki ya soko la pamoja la EAC, ambayo inahakikisha uruhu wa watu kusafiri, kuhudumu na haki ya kuanzishwa kwa biashara na raia wa mataifa ya afrika mashariki.
Aidha Kenya iliasema imeandika rasmi barua kwa EAC kuiarifu rasmi jamhuri ya muungano wa Tanzania kuangazia upya agizo hilo ili kuhakikisha inafuata kikamilifu mkataba wa EAC na sheria za Jumuia.
Maafisa wa EAC kwa sasa wanafanya uchambuzi wa hatua hiyo na itawasilisha hatua zozote zilizokiukwa pamoja na kaununi zilizopo katika mkutano ujao wa baraza la kisekta la biashara, viwanda na uekezaji.
Taarifa ya Joseph Jira