News
Mpango wa Skills Mtaani kufaidi vijana 600 Malindi.

Jumla ya vijana 600 kutoka eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi watanufaika na mpango wa mafunzo ya taaluma za ujuzi, maarufu SKILLS MTAANI unaofadhiliwa na mbunge wa Malindi Amina Mnyazi.
Akizungumza na wanahabari mjini humo, Mnyazi alidokeza kuwa mpango huo utakaotekelezwa kupitia vyuo vya kiufundi vilivyo katika eneo hilo unalenga vijana walio mitaani ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kujistawisha.
Mnyazi alikariri kuwa mpango huo pia utasaidia kupunguza visa vya utovu wa usalama vinavyoshuhudiwa mjini humo kwa kuwapa vijana ujuzi wa kujishughulisha katika jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi kutoka eneo la Kijiwetanga wakiongozwa na Esther Mathias na Katao Nzai Joseph waliupongeza mpango huo wakisema utasaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kupunguza uhalifu katika jamii.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi