News
Migos: Serikali yajipanga kwa mpito wa Junior Secondary Januari, 2026

Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alisema serikali ya kitaifa imejiandaa kikamilifu kwa mpito wa wanafunzi kuingia Sekondari ya Juu (Junior Secondary), Januari 2026.
Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Embu, Waziri Migos alisema kuwa mikakati imewekwa kuhakikisha wanafunzi wa Gredi ya 10 hawakosi masomo wanapojiunga na shule hizo.
Aliongeza kwamba serikali imewekeza katika ujenzi wa miundombinu, hasa madarasa ili kuhakikisha shule zinakuwa tayari kwa mapokezi ya wanafunzi hao.
Hata hivyo, wadau wa elimu walielezea wasiwasi wao kuhusu utayari wa serikali, hasa katika masuala ya miundombinu ya shule, ufadhili wa wanafunzi, upatikanaji wa vitabu, maabara, mafunzo kwa walimu na uratibu wa mikondo mitatu ya masomo kama ilivyopangwa.
“Kama serikali, tumejiandaa kupokea watoto wetu kutoka Gredi ya 9 hadi 10. Wanafunzi wameshaanza kuchagua kati ya mikondo mitatu ya masomo na shule, na tumehakikisha zoezi hilo linakamilika kwa ufasaha,” alisema Waziri Migos.
Taarifa ya Elizabeth Mwende.
News
Wahudumu wa afya Lamu watishia kuishtaki serikali ya kaunti hiyo

Wahudumu wa Afya kaunti ya Lamu wametishia kuelekea Mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti hiyo kwa kukaidi kutekeleza matakwa yao.
Wahudumu hao waliishtumu serikali ya kaunti ya Lamu kwa kupuuza matakwa yao na badala yake kutumia vitisho ili kuwashurutisha kurejea kazini.
Kulingana na viongozi wa wahudumu hao, licha ya mgomo wao kuendelea kwa zaidi ya wiki mbili serikali ya kaunti hiyo imekataa kata kuandaa vikao vya kusuluhisha malalamishi yao.
Baadhi ya changamoto wanazolalamikia ni pamoja na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kupandishwa vyeo, kupuuzwa kwa mkataba wa makubaliano ya nyongeza ya mishahara, kunyimwa kwa mishahara kwa baadhi ya wahudumu hao miongoni mwa matakwa mengine.
“Mkiendelea kutufinyilia itabidi tufuate njia ya sheria kwa sababu tunajua tunalilia haki yetu, haiwezekani serikali ya kaunti inashindwa kutupandisha vyeo ilhali tumefanya kazi kwa miaka 15 sasa, hatuwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira duni na pia mkataba wa makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara sharti itekelezwe” walisisitiza viongozi hao.
Wakati uo huo serikali ya kaunti ya Lamu imejibu malimishi yao kupitia barua na kutangaza kuwa mgomu huo ni kinyume cha seria na kuwataka wahudumu hao kurejea kazini mara moja.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Rais Ruto atuma KDF kusimamia ujenzi wa hospitali nchini

Rais William Ruto ametuma jeshi la KDF kusimamia ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 75 kote nchini katika juhudi za kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa haraka.
Akizungumza katika kaunti ya Narok wakati wa uzinduzi wa hospitali ya Sogoo Level 4, waziri wa ulinzi Patrick Mariru alifichua kuwa ujenzi wa hospitali hiyo yenye mamlaka kamili itakamilika baada ya mda wa miezi 11.
Ujenzi wa hospitali ya Sogoo Level 4 ulivutia rais Ruto alipozuru eneo hilo mwezi mei mwaka 2025, jambo lililomfanya kuagiza KDF kuipandisha hadhi.
Mariru hata hivyo alishikilia kuwa wafanyikazi wote wasio na ujuzi watatolewa kutoka kwa jamii.
“Jeshi litamsimamia mkandarasi. Hilo liwe wazi, kazi yote itafanywa na vijana wa Sogoo. Tutaweka maafisa wawili na kila jioni watanipa ripoti ya maendeleo,” alisema Mariru.
“Tuna zaidi ya miradi 75 tunayosimamia na sio kwamba tunabadilisha wakala wa serikali tunataka tu kushirikiana na ofisi tofauti miongoni mwao wizara za afya na michezo.”
Taarifa ya Joseph Jira