News
Mboko: Dhulma za kijinsia dhidi ya watoto lazima zikomeshwe

Mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko amewakosoa baadhi ya wakaazi wa eneo bunge hilo kwa madai ya kukosa kuchukulia kwa uzito kesi za dhulma za kijinsia dhidi ya watoto.
Bi Mboko alisema vitendo hivyo vinakiuka haki za mtoto na wenyeji wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanadhibiti visa hivyo.
Bi Mboko ambaye alikuwa akizungumza katika eneo bunge lake la Likoni, alisema kuna haja ya wakaazi kuripoti visa hivyo kwa asasi za kiuslama ili washukiwa wa visa hivyo wakabiliwe kisheria.
“Hizi kesi za Femicide na GBV kwa nini ushahidi upotee polisi, ati evidence hakuna na mtoto ameletwa akiwa yuko katika zile hali na kila kitu alafu ati ushahidi unapotea, please handle these cases with the heart of humanity’’, alisema Bi Mboko.
Vilevile, aliwahimiza maafisa wa polisi kuwajibika vilivyo pindi kesi hizo zinaporipotiwa kwao.
Wakati huo huo, alitoa wito kwa wenyeji wa Likoni kushirikiana na vitengo vya usalama ili kudhibiti visa vya watoto wenye umri mdogo kujiungiza katika uhalifu na kuhakikisha watoto hao wanapelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Chrispus aomba msahama bunge la kaunti ya Taita Taveta

Mwakilishi wadi ya Bomani mjini Taveta kaunti ya Taita Taveta Chrispus Tondoo ameliomba bunge la kaunti hiyo msamaha kutokana na matamshi aliyoyatoa hapo awali akikashifu bunge hilo kwa madai ya kushamiri kwa visa vya ufisadi na utepetevu.
Tondoo akiomba msamaha katika bunge hilo alisema alitambua athari zilizosababishwa na matamshi hayo kwa wenyeji wa kaunti hiyo na bunge hilo, hali ambayo imemfanya kuchukua hatua hiyo ya kuomba msamaha.
Aidha Tondoo aliahidi kuliheshimu bunge hilo kwa mujibu wa kanuni na Sheria za bunge la kaunti ya Taita Taveta.
‘’Naomba msamaha kutokana na matamshi ambayo niliyatoa tarehe 2 na tarehe 3 mwezi wa Juni mwaka huu wa 2025 kwani hayakuwa yenye heshima kwa wenyeji wa Taita Taveta na bunge la kaunti’’, alisema Tondoo.
Tondoo alikuwa Mwakikishi wa wadi wa pili kuomba msamaha baada ya Mwakilishi wa wadi ya Kaloleni mjini Voi Ahmed Azari kuchukua hatua hiyo mwezi mmoja uliyopita.
Haya yalijiri baada ya kaimu spika wa bunge hilo Anselim Mwadime kuapa kuwachulia hatua za kisheria wanachama wanne wa bunge hilo, wawili wakiwa ni Tondoo na Azari ambayo tayari wameomba msamaha huku wawili wakiwa wamesalia bila kuomba msamaha.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mawakili Kilifi waungana kushtumu mauaji ya Wakili Mbobu

Siku chache baada ya Wakili Kyalo Mbobu kuuawa kinyama kwa kupigwa risasi mara kadhaa akiwa kwenye gari lake barabara ya Lang’ata jijini Nairobi, mawakili mjini Kilifi kaunti ya Kilifi wameungana na mawakili wengine nchini siku ya Ijumaa Semtemba 12 mwaka huu kufanya matembezi ya amani, wakishutumu vikali mauaji hayo.
Wakiongozwa na Mwakilishi wao Sesil Mila, mawakili hao walilaani vikali mauaji ya wakili Mbobu wakiishutumu serikali kwa kutowajibikia swala la usalama wa wananchi wake.
Aidha waliitaka idara ya usalama kuhakikisha kuwa inafanikisha wajibu wake wa kuwalinda mawakili wakisisitiza haja ya haki kupatikana kwa familia ya mwendazake wakili Kyalo.

Mawakili wa Kilifi wakiongozwa na Sesil Mila, washtumu mauaji ya Wakili Kyalo Mbobu
Mawakili hao sasa waliitaka idara ya upelezi na asasi zote husika kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina unafanywa kubaini watuhumiwa wa mauaji hayo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya Hamis Kombe