News
Mamlaka ya CA yasitisha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano

Serikali imeagiza vituo vyote vya habari vya runinga za kitaifa na radio kusitisha mara moja matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya mawasiliano nchini CA na kutiwa saini na Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo David Mugonyi, ilisema kituo chochote za habari kitakachokiuka agizo kitachukuliwa hatua za kisheria.
Mamlaka ya CA ilisema baada ya kufuatilia kwa makini matukio yote yanayoendelea katika maandamano hayo, wamebaini kwamba maandamano hayo yamekiuka kipengele cha 33 ibara ya 2 na kipengele cha 34 ibara ya kwanza ya Katiba.
CA ilidai kwamba maandamano hayo pia yameenda kinyume na kifungu cha 461 cha sheria za habari na mawasiliano nchini.

Picha kwa hisani
Wakati huo huo Mamlaka hiyo iliweka wazi kwamba itaendelea kufuatilia taarifa zote zinazopeperushwa katika runinga na Radio ili kuhakikisha zinazingatia sheria na kanuni za habari na mawasiliano.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira