News
Mahakama ya Kilifi Imemhukumu Kaingu miaka 13 jela

MAHAKAMANI-
Mahakama ya Kilifi imemhukumu kifungo cha miaka 13 gerezani mwanamume wa umri wa makamu baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa umri wa miaka 9.
Hakimu wa Mahakama ya Kilifi Ivy Wasike amesema mshukiwa Harrison Kaingu Ngolo ana muda wa siku 14 pekee wa kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama.
Awali kabla ya uamuzi huo kutolewa, Mahakama imeelezwa kwamba mshukiwa alitekeleza kitendo hicho mnamo tarehe 1 mwezi Aprili mwaka 2022 katika eneo la Shingila kaunti ya Kilifi.
Mahakama pia imeelezwa kwamba mshukiwa alitekeleza unyama huo baada ya kumtuma mtoto huyo amletee maandazi kwake nyumbani ndiposa alitumia nafasi hiyo kumnyanyasa haki zake mtoto huyo.
Mahakama hata hivyo amefafanua kwamba hukumu hiyo imezingatia afya ya mtoto kwani ni miaka 3 sasa baada ya kitendo hicho, mtoto huyo bado anahisi maumivu.
News
Wazee wa Kaya wanataka bunge kupitisha sheria kudhibiti mauaji ya wazee

Muungano wa Wazee wa Kaya kaunti ya Kilifi umeitaka serikali kuu kupitia bunge la kitaifa kubadilisha sheria ya mwaka wa 1926 kuhusu uchawi ili kuwezesha utamaduni kudhibiti mauaji ya wazee yanayoendelea kushuhudiwa kaunti ya Kilifi.
Wakiongozwa na Stanley Kahindi Kiraga wamesema kuwa sheria hiyo imechangia pakubwa mauaji ya wakongwe Kilifi kutokana na swala kuwa haitambui uwepo wa uchawi na jinsi ya kuudhibiti.
Kiraga sasa anasema ni sharti sheria hiyo iondolewe au ifanyiwe ukarabati bungeni hali itayopelekea uchawi kudhibitiwa kupitia mila na utamaduni.
“Vijana wanaowaua wazee wakiwasingizia kuwa wachawi wanazidi kuongezeka na kwa sababu hakuna sheria ya moja kwa moja ya kuwashtaki na kuwafunga” amesema Kiraga akieleza kusikitishwa kwake na ongezeko la magenge ya vijana wanaolipwa kutekelezwa mauaji ya wazee kwa shutuma za uchawi.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Mahakama ya Kilifi yaanzisha upya kesi ya ulaghai wa pesa

Mahakama ya Kilifi imeanzisha upya kesi ya mwanaume mmoja anayekabiliwa na shtaka la ulaghai wa pesa.
Hii ni baada ya Mwanaume huyo kwa jina Samuel Ngonyo, kuachiliwa kwa dhamana hapo awali lakini alikosa kudhuhuria vikao Mahakamani hali iliyopelekea kesi hiyo kuanzishwa upya.
Hakimu mkuu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa aliagiza jamaa huyo kuzuliwa rumande baada ya agizo la kukamatwa kwake kuidhinishwa na Mahakama baada ya jamaa huyo kupuuza vikao vya Mahakama vya awali.
Kabla ya agizo hilo, Mahakama ilielezwa kwamba mnamo tarehe tofauti kati ya mwezi Septemba hadi Oktoba mwaka 2021 katika maeneo la Ganze kaunti ya Kilifi kwa kutumia njia ya ulaghai, mshukiwa alichukua pesa taslimu shilingi elfu 50 ya mlalamishi Grace Sidi Katana.
Mahakama ilielezwa zaidi kwamba mshukiwa alitekeleza kitendo hicho baada kumdanganya Mlalamishi kwamba yeye ni Mwandishi na afisa wa kazi za umma hivyo angemsaidia Moses Katana mtoto wa mlalamishi kupata kazi ya serikali.
Kesi hiyo itaendelea mnamo tarehe 13 mwezi Agosti mwaka huu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu