News
Mahakama ya Kilifi Imemhukumu Kaingu miaka 13 jela

MAHAKAMANI-
Mahakama ya Kilifi imemhukumu kifungo cha miaka 13 gerezani mwanamume wa umri wa makamu baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa umri wa miaka 9.
Hakimu wa Mahakama ya Kilifi Ivy Wasike amesema mshukiwa Harrison Kaingu Ngolo ana muda wa siku 14 pekee wa kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama.
Awali kabla ya uamuzi huo kutolewa, Mahakama imeelezwa kwamba mshukiwa alitekeleza kitendo hicho mnamo tarehe 1 mwezi Aprili mwaka 2022 katika eneo la Shingila kaunti ya Kilifi.
Mahakama pia imeelezwa kwamba mshukiwa alitekeleza unyama huo baada ya kumtuma mtoto huyo amletee maandazi kwake nyumbani ndiposa alitumia nafasi hiyo kumnyanyasa haki zake mtoto huyo.
Mahakama hata hivyo amefafanua kwamba hukumu hiyo imezingatia afya ya mtoto kwani ni miaka 3 sasa baada ya kitendo hicho, mtoto huyo bado anahisi maumivu.
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi