News
KUPPET na KNUT washinikiza nyongeza ya mshahara

Chama cha Walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri nchini KUPPET, kimeionya Tume ya uajiri walimu nchini TSC dhidi ya kuwasilisha pendekezo lipya linalokinzana na mkataba wa makubaliano wa malipo wa CBA wa mwaka wa 2025-2029.
Katibu mkuu wa KUPPET nchini, Akello Misori alisisitiza kwamba kuna haja ya kutathiminiwa upya kwa marupurupu yote ya walimu, akisema ni lazima mkataba huo unaangaliwe.
Akello alisema ili kuwawezesha walimu kutekeleza makujumu yao vyema, ni lazima serikali kupitia Tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuangalia upya mkataba uliopo mezani na kuhakikisha matakwa ya walimu yanatekelezwa.
“Hivi karibuni kutatua na mazungumzo na muajiri wetu na sisi tuko na msimamo kwamba ni lazima nyongeza ya mshahara ya asilimia 50 na marupurupu ya walimu wanaofanyakazi katika mazingira magumu ya asilimia 30 pia iangaliwe upya”, alisema Akello.
Hata hivyo katika hafla tofauti, Naibu Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha walimu nchini KNUT Aggrey Namisi alisema iwapo hakutakuwa na mwafaka wowote kuhusu pendekezo hilo la CBA basi wataitisha mgomo wa kitaifa kuanzia mwezi Agosti.
“Sisi tuko tayari kufanya kazi lakini pia matakwa yetu ni lazima yaangaziwe na tunaiambia TSC kama itaendelea kugairi mambo yetu ya CBA mpya tutaambia walimu waanze mgomo mwezi Agosti na watakaoumia na wanafunzi wa gredi ya 9”, alisema Namisi.

Katibu mkuu wa KNUT Collins Oyoo
KUPPET na KNUT hata hivyo wanalenga kuweka mezani mahitaji mapya ya walimu wakati wa mazungumzo kati ya serikali na viongozi wakuu wa vyama hivyo huku suala la nyongeza ya mishahara na marupurupu ya asilimia 50 likipewa kipau mbele.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Wahudumu wa afya Lamu watishia kuishtaki serikali ya kaunti hiyo

Wahudumu wa Afya kaunti ya Lamu wametishia kuelekea Mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti hiyo kwa kukaidi kutekeleza matakwa yao.
Wahudumu hao waliishtumu serikali ya kaunti ya Lamu kwa kupuuza matakwa yao na badala yake kutumia vitisho ili kuwashurutisha kurejea kazini.
Kulingana na viongozi wa wahudumu hao, licha ya mgomo wao kuendelea kwa zaidi ya wiki mbili serikali ya kaunti hiyo imekataa kata kuandaa vikao vya kusuluhisha malalamishi yao.
Baadhi ya changamoto wanazolalamikia ni pamoja na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kupandishwa vyeo, kupuuzwa kwa mkataba wa makubaliano ya nyongeza ya mishahara, kunyimwa kwa mishahara kwa baadhi ya wahudumu hao miongoni mwa matakwa mengine.
“Mkiendelea kutufinyilia itabidi tufuate njia ya sheria kwa sababu tunajua tunalilia haki yetu, haiwezekani serikali ya kaunti inashindwa kutupandisha vyeo ilhali tumefanya kazi kwa miaka 15 sasa, hatuwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira duni na pia mkataba wa makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara sharti itekelezwe” walisisitiza viongozi hao.
Wakati uo huo serikali ya kaunti ya Lamu imejibu malimishi yao kupitia barua na kutangaza kuwa mgomu huo ni kinyume cha seria na kuwataka wahudumu hao kurejea kazini mara moja.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Rais Ruto atuma KDF kusimamia ujenzi wa hospitali nchini

Rais William Ruto ametuma jeshi la KDF kusimamia ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 75 kote nchini katika juhudi za kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa haraka.
Akizungumza katika kaunti ya Narok wakati wa uzinduzi wa hospitali ya Sogoo Level 4, waziri wa ulinzi Patrick Mariru alifichua kuwa ujenzi wa hospitali hiyo yenye mamlaka kamili itakamilika baada ya mda wa miezi 11.
Ujenzi wa hospitali ya Sogoo Level 4 ulivutia rais Ruto alipozuru eneo hilo mwezi mei mwaka 2025, jambo lililomfanya kuagiza KDF kuipandisha hadhi.
Mariru hata hivyo alishikilia kuwa wafanyikazi wote wasio na ujuzi watatolewa kutoka kwa jamii.
“Jeshi litamsimamia mkandarasi. Hilo liwe wazi, kazi yote itafanywa na vijana wa Sogoo. Tutaweka maafisa wawili na kila jioni watanipa ripoti ya maendeleo,” alisema Mariru.
“Tuna zaidi ya miradi 75 tunayosimamia na sio kwamba tunabadilisha wakala wa serikali tunataka tu kushirikiana na ofisi tofauti miongoni mwao wizara za afya na michezo.”
Taarifa ya Joseph Jira