Business
KPA kushirikiana na kaunti ya Siaya kibiashara

Halmashauri ya bandari Kenya (KPA) pamoja na serikali ya kaunti ya Siaya zimeahidi kushirikiana kwa karibu kuimarisha miundomsingi ya usafiri na biashara katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Katika kikao cha viongozi wa pande zote mbili kilichofanyika jijini Mombasa, viongozi hao walijadili miradi ya miundomsingi ya baharini inayolenga kufungua fursa mpya za uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ya Ziwa Victoria.
Mkurugenzi mkuu wa KPA nahodha William Ruto alithibitisha kuwa usanifu wa kivuko cha Usenge utakamilika ndani ya wiki mbili, huku ikiahidi kushirikiana na Kenya Shipyards Limited kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati.
Aidha, Ruto alieeleza utayari wa mamlaka hiyo kushirikiana na serikali ya kaunti ya Siaya kuhakikisha miradi hiyo inaendana na vipaumbele vya eneo hilo.
Ruto aliongeza kuwa miradi hiyo inalenga kuchochea uwekezaji, kuongeza nafasi za ajira na kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika ukanda wa ziwa.
Kwa upande wake, gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo alieleza kuridhishwa na ushirikiano huo, akimpongeza nahodha Ruto kwa uongozi wake wa vitendo akisema kuwa miradi hiyo inaleta matumaini mapya kwa wakazi wa Siaya na ukanda mzima wa Ziwa Victoria.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
Business
Mradi wa kiuchumi wa Dongo Kundu wavutia wawekezaji zaidi

Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaendelea kuonyesha nia ya kuekeza katika mradi wa kiuchumi wa dongo kundu kaunti ya Mombasa.
Mradi huo unaotarajiwa kuongeza uzalishaji katika viwanda na thamani ya bidhaa ndani ya nchi na nje, unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Kampuni ya nishati kutoka China, Ruike Energy Group Limited, ni mwekezaji wa hivi karibuni kuonyesha nia ya kupata nafasi ndani ya eneo hilo la kiuchumi la Dongo Kundu kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta.
Kulingana na halmashauri ya bandari nchini KPA hatua hiyo italeta faida Zaidi ikiwemo kubuni nafasi za ajira, ikuaji wa uchumi, upatikanaji wa vifaa vya baharini, na urahisi wa kufikia masoko ya kanda na ya kimataifa.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
KETRACO kuimarisha usalama wa chakula nchini

Shirika la usambazaji umeme nchini, KETRACO, limethibitisha dhamira yake ya kuimarisha usalama wa chakula, ukuaji wa kijani, na ushirikiano wa kieneo kupitia uekezaji mkubwa katika miundombinu ya umeme.
Katika maonesho ya Kimataifa ya kilimo ASK yanayoendelea kaunti ya Mombasa, KETRACO imeonyesha jinsi miundombinu yake ya umeme inavyowezesha kilimo cha kisasa na uzalishaji wa viwandani.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi mkuu, mhandisi Kipkemoi Kibias, KETRACO imekamilisha miradi 43 ya njia za kusafirisha umeme, huku mingine 29 ikitarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2028.
Kibias, alisema shirika hilo tayari limejenga zaidi ya kilomita elfu sita za njia za umeme wa msongo mkubwa, likiwa pia na vituo 46 vya kusambaza umeme na upanuzi wa mitambo 33.
Katika eneo la Pwani, Kibias alisema upanuzi wa mpango wa Green Energy Backbone umewezesha usambazaji wa kawi safi kwa asilimia 93, jambo lililopunguza utegemezi wa mafuta na kuchochea maendeleo ya biashara za kilimo, utalii na uchumi wa baharini.
Kibias alisema KETRACO inaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuunganisha Kenya na nchi jirani kupitia njia za kimataifa kama zile za Ethiopia, Tanzania na Uganda hatua zitakazowezesha biashara ya umeme Afrika Mashariki.
Taarifa ya Mwanahabari wetu