News
KMPDU yaonya madaktari wazembe pwani

Muungano wa madaktari nchini KMPDU tawi la pwani umeonya madaktari wazembe ukisema hautamtetea daktari yeyote atakayepatikana anakwepa majukumu yake.
Hii ni baada ya taarifa ya kamati ya afya ya bunge la seneti katika ziara yao kwenye hospitali ya rufaa ya Kilifi, kudai walikosa kuwaona baadhi ya madaktari waliopaswa kuwa kazini wakati huo.
Mwenyekiti wa KMPDU eneo la Pwani Daktari Niko Gichana alisema usimamizi wa kaunti unafaa kueleza chanzo cha madaktari hao kutokuwa kazini.
Gichana aliongeza kuwa hospitali za umma zinakumbwa na uhaba mkubwa wa madaktari na kusababisha waliopo kufanya kazi kwa mda mrefu bila mapumziko.
Afisa huyo alishauri usimamizi wa kaunti ya Kilifi kushughulikia suala la uajiri wa madaktari zaidi.
Kamati hiyo ikiongozwa na seneta David Wakoli Wafula ilibaini kuwepo dawa za matibabu zilizopitwa na wakati, baadhi ya madaktari kutofika kazini pamoja na hali duni ya usafi hospitalini wakati ilipozuru taasisi hiyo ya afya.
Ilimtaka gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro kuwachukulia hatua za kinidhamu wahudumu wa afya waliokwepwa majukumu.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.