News
Kikao cha umma chazua mvutano Msambweni

Mkutano wa ukusanyaji maoni ya umma kaunti ya Kwale kuhusiana na pendekezo la kuongezwa kwa ada za kuingia katika mbuga za wanyamapori nchini uliibua hisia mseto miongoni mwa wenyeji wa kaunti ya Kwale.
Mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la huduma kwa wanyamapori nchini KWS eneo la Bongwe ulitibuka baada ya viongozi wa kisiasa na wakaazi wanaoendeleza shughuli zao katika fuo za bahari kudai kuwa serikali ina njama ya kunyakuwa eneo la Diani Chale Marine Reserve.
Wakiongozwa na mbunge wa Msambweni kaunti ya Kwale Feisal Bader, Madai ya wakaazi hao yalijiri kufuatia tangazo la hapo awali lililochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa eneo hilo linafaa kuwa katika himaya ya KWS.
“Sisi kama Wananchi wa Msambweni tunasema maoni yetu tunayatoa kuwa tunaanza rasmi mchakato kuhusu eneo la Diani Marine reserve’’, alisema Bader.

Mbunge wa Msamweni Feisal Bader akihutubia wakaazi wa Msambweni
Hata hivyo naibu Mkurugenzi wa uhifadhi eneo la Pwani Elema Hapisha alisema shughuli hiyo inayoendelea katika maeneo tofauti nchini haihusiani kivyovyote na utata unaojiri kuhusu usimamizi wa eneo la Diani Chale Marine Reserve.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.