News
Kampeni ya Chanjo kwa watoto yafanikiwa nchini

Wizara ya afya nchini imesema kufikia sasa watoto milioni 3.3 wamepokezwa chanjo ya surua kati ya watoto milioni 6.5 waliolengwa.
Ripoti ya wizara hiyo pia iliongeza kuwa watoto milioni 12.1 wamepokea chanjo ya homa ya matumbo kati ya waliolengwa milioni 19.2.
Vile vile ripoti hiyo ilisema kuwa zaidi ya watoto elfu nne ambao walikuwa hawajapokea chanjo yeyote awali sasa wamefanikiwa kuchanjwa.
Wizara hiyo iliongeza kuwa kampeni hiyo ya kitaifa ya chanjo iliyoanza tarehe 5 Julai, 2025, imepokelewa vyema na wazazi, viongozi wa dini, walezi, wahudumu wa afya na wakenya kwa jumla.
Wizara hiyo ilishauri wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapewa chanjo hiyo ikiwa zimesalia siku tatu pekee kabla kampeni kuu kukamilika.
Chanjo hizo zimeidhinishwa na shirikala afya dunia WHO na zimethibitshwa kuwa salama, bora na huokoa maisha.
Waziri wa afya Aden Duale alisema serikali imejitolea kuhakikisha hakuna mtoto atakayepoteza maisha kwa ugonjwa unaoweza kuzuilika kwa Chanjo.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira