News
Kalonzo ataka serikali kufafanua kuhusu uwepo wa maafisa wa Jubaland nchini.

Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Msyoka ameitaka serikali ya rais William Ruto kutoa ufafanuzi kuhusu uwepo wa maafisa kutoka Jubaland hapa nchini.
Kalonzo alisema hatua hiyo inazua maswali mazito kuhusu usalama wa taifa.
Kinara huyo aliongeza kuwa hali ya usalama nchini imeendelea kutatizika huku raia wa maeneo ya mipakani kama Mandera wakiishi kwa hofu ya kuhatarisha maisha yao.
Alisema kitendo cha maafisa wa usalama kutoka taifa jirani kuwepo hapa nchini bila maelezo ya wazi kinaweza kuchochea mzozo wa kiusalama na kuathiri utulivu wa kitaifa.
Viongozi wa kisiasa na wananchi walieleza wasiwasi wao kuhusu athari za hali hiyo wakitaka serikali kutoa maelezo ya kina na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mipaka ya nchi inalindwa ipasavyo.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.