News
Gavana Mung’aro aapa kukabiliana na matabibu wazembe

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Maitha Mung’aro amesema muungano wa madaktari nchini KMPDU umekua kikwazo kikubwa katika kulainisha utendakazi wa madaktari.
Gavana Mung’aro alisema muungano huo wa kutetea maslahi ya madaktari nchini umelemaza huduma za matibabu hasa katika hospitali za umma.
Akizungumza na wanahabari katika makaazi yake, gavana Mung’aro alitishia kuwachukulia hatua kali madaktari wazembe na wale wanaosusia kazi mara kwa mara huku wakihudumu katika hospitali za kibinafsi.
Vile vile gavana huyo aliokeza kuwa wizara ya afya inalenga kuajiri madakrati wa kliniki wapya ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Haya yanajiri baada ya kamati ya afya ya bunge la seneti kuzuru hospitali ya rufaa ya Kilifi mjini Kilifi na kuwakosa baadhi ya madaktari waliopaswa kuwa kazini.
“Mimi mwenyewe sikwenda pamoja na nyinyi wakati mlikua mnatembelea hospitali hizo lakini nafurahi kwa sababu mmejionea wenyewe kwamba matabibu wengi wanafanya kazi katika hospitali za kibinafsi wanakuja kazini pindi tu wanapopigiwa simu kwamba kuna mgonjwa, na nitahakikisha imekomesha hii tabia”, alionya gavana Mung’aro.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi

Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa wanaume 6 wanaokabiliwa na mashtaka ya unajisi.
Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike alimhukumu Lucky Munga na Hassan Daniel kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya Mahakama kubaini kwamba walihusika kwa kuwatendea unyama watoto wa umri wa miaka 13 na 15.
Safari Karisa Lewa alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kumnajisi mtoto wake mwenyewe wa umri wa miaka 14 huku Eric Ruwa na Lucky Katana Kenga wakihukumiwa kifungo cha miaka 6 gerezani kwa kosa sawa na hilo.
Hata hivyo Mahakama hiyo ilimhukumu kifungo cha miaka 3 Kithi Kombe kutokana na kesi hiyo kwa mtoto wa miaka 15, japo baadaye Mahakama ikabaini kwamba mshukiwa sio baba halali wa mtoto aliyezaliwa baada ya Kithi kumnajisi mtoto huyo.
Akizungumza wakati wa vikao vya Mahakama baada ya kutoa hukumu hizo, Hakimu Wasike alisema Mahakama umezingatia ushahidi uliyotolewa Mahakamani huku akiwarai wananchi kujitenga na visawishi vibaya ili kuepuka mkono wa sheria.
Hakimu Wasike alihoji kwamba washtakiwa wa haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama lakini kwa kuzingatia taratibu zote za Mahakama na sheria.
Taarifa ya Teclar Yeri
News
Thoya: Serikali kuu iongeze mgao wa fedha kwa sekta ya Afya

Naibu gavana wa kaunti ya Mombasa Francis Thoya ametoa changamoto kwa serikali kuu kuongeza mgao wa fedha ili kufanikisha utaoji wa huduma za afya.
Akizungumza katika kaunti hiyo, Thoya alisema kuwa huduma nyingi za afya katika kaunti hiyo ya Mombasa zinakabiliwa na changamoto ya raslimali ndogo hali ambayo inakwamisha juhudi za kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Thoya pia alitaka serikali kuhakikisha inaharakisha kuajiri wahudumu zaidi wa afya ili wenyeji wa Mombasa waweze kupata huduma bora za matibabu bila changamoto zozote.
Aidha, Thoya alisema kwamba hali ya uhaba wa wahudumu wa afya ni changamoto kuu ambayo inazuia utoaji wa huduma bora za matibabu hali inayowafanya wale wachache waliopo kufanya kazi katika mazingira magumu.
Taarifa ya Janet Mumbi