News
Fikirini Jacobs: Serikali kuimarisha vijana kibiashara

Katibu katika idara ya vijana na uchumi bunifu nchini Fikirini Jacobs amesema serikali imeweka mikakati kabambe ya kubuni ajira kwa vijana kupitia miradi ya kibiashara.
Akizungumza na Coco Fm, Jacobs alisema vijana ambao hawakamilisha elimu ya sekondari, wameangaziwa katika mradi wa kibiashara uitwao Nyota ambao serikali imeekeza pesa za kutosha.
Jacobs amedokeza kuwa mpango huo unaolenga vijana 100,000 utazinduliwa hivi karibuni nchini na vijana 70 katika kila wadi nchini watafaidi.
Alidokeza kuwa tayari idadi kubwa ya vijana wametuma maombi ya kusajiliwa katika mpango huo.
“Sehemu ya kwanza kutegemea na vile ambavyo zilitangazwa inaitwa Business Support, ni sehemu ambayo mhesimiwa rais alitangaza hata akiwa siku ya madaraka kule Homabay kwamba kumewekwa shilingi bilioni tano kati ya hizi bilioni zote ambazo lengo lake ni kuenda kusaidia vijana laki moja ambao ni vijana 70 kwa kila wadi ya Kenya”, alisema Fikirini
Pia alisema kuwa vijana wanaoishi na ulemavu nchini wamezingatiwa katika mpango huo katika juhudi za kuafikia usawa.
Vile vile alisema serikali imejenga vituo 155 vya kuwezesha kiujuzi vijana katika maeneo bunge yote nchini akidokeza kuwa kaunti ya Kilifi kuna vituo viwili zaidi ambavyo vitajengwa.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.