News
Chibule, awahimiza wakaazi kuzingatia uhifadhi wa mazingira

Naibu Gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule, aliwahimiza wenyeji wa kaunti ya Kilifi kuwa mstari wa mbele kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yalifanyika siku ya Alhamisi tarehe 5 Juni, 2025, katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi kaunti ya Kilifi, Chibule alisema hamasa zinapaswa kutolewa kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
Aidha alisisitiza haja ya jamii kuzingatia usafi wa mazingira ili kuzuia mkurupuko wa magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.
“Kuna haja ya wazazi pamoja na walimu kuweka mikakati ya kuwaelimisha watoto umuhimu wa utunzaji mazingira na sio kuachia Mashirika na wadau wa mazingira jukumu hili” Alisema Chibule.
Naibu Gavana wa Kilifi Flora Mbetsa Chibule akipamba miti
Vilevile, Chibule alisema watalii wamekuwa wakizuru kaunti ya Kilifi kutokana na mazingira safi na kushinikiza uchakataji wa chupa za plastiki.
Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa mazingira walitoa wito swa serikali ya kaunti ya Kilifi kutenga kipande cha ardhi ambacho kitatumika kwa utupaji wa taka za plastiki.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira