News
Chibule, ahimiza wakaazi kutoa damu kusaidia wagonjwa wa Selimundu

Wizara ya afya kaunti ya Kilifi imefichua kwamba maradhi ya Selimundu ni miongoni mwa maradhi ambayo yanaathiri idadi kubwa zaidi ya wakaazi kaunti hiyo.
Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Afya kaunti hiyo Peter Mwarogo, mkurugenzi wa afya kaunti ya Kilifi Leli Hassan alisema kwamba kila siku zaidi ya watu kumi hupatikana wakiugua maradhi hayo kaunti ya Kilifi.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya maradhi hayo ya Selimundu katika uwanja wa Vipingo eneo bunge la Kilifi Kusini kaunti ya Kilifi, wizara hiyo imesema kwamba asilimia sitini ya maradhi hayo yameathiri wakaazi wa eneo bunge la Kilifi Kusini.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Naibu Gavana kaunti ya Kilifi Florah Mbetsa Chibule ambaye alisisitiza haja ya wakaazi kujitokeza na kutoa damu kwa hiari ili kuhakikisha wanasaidia waathiriwa wanaougua maradhi ya Selimundu.

Wananchi wakishiriki maandimisho ya siku ya Selimundu
Vile vila Chibule alisitiza haja ya wakaazi kujisahili kwenye mpango wa bima ya Kitaifa ya afya SHA ili kupata matibabu ya gharama ya chini wanapotaka dharura ya kiafya.
Naibu gavana huyo alisistiza jamii kaunti hiyo kuondoa unyanyapaa kwa waathiriwa wa maradhi hayo huku akishinikiza hamasa kwa jamii kuhusu kwa watu wanaoishi na maradhi hayo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya afya ya jamii Bashir Isaak akizungumza kwa niaba ya waziri wa afya nchini Aden Duale, alisema eneo la pwani na magharibi mwa nchi ndiyo yaliyosajili idadi kubwa ya wanaoishi na maradhi hayo.
Bashiri alipendekeza wahudumu wa afya nyanjani kupewa mafunzo maalumu ya kuhakikisha wanatambua sawa na kuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa waathiriwa wa maradhi hayo hasa maeneo ya mashinani.
Alisistiza haja ya waathiriwa wa maradhi hayo na umma kwa ujumla kujisajili kwenye mpango wa bima ya matibabu ya afya wa SHA ili kuwagharamia matibabu kwani baadhi ya wanaougia maradhi hayo hawana uwezo wa kimatibabu sawa na kununua dawa.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mahakama ya Malindi yawaachilia washukiwa 3 wa kesi ya Kwa Binzaro

Mahakama Kuu ya Malindi imewaachilia washukiwa watatu wanaohusishwa na kesi ya mauaji ya halaki ya watu katika kijiji cha Kwa Binzaro eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.
Hakimu wa Mahakama hiyo Joy Wesonga aliagiza kuachiliwa huru kwa Safari Kenga Nzai, Gona Charo Kalama na Kahindi Kazungu Garama wote wakiwa wakaazi wa kijiji hicho cha Kwa Binzaro.
Watatu hao walikuwa wamekamatwa baada ya kudaiwa kuuza shamba la ekari tano kwa mshukuwa mkuu wa mauaji ya watu katika kijiji cha Kwa Binzaro Sherleen Temba Anido.
Hakimu Wesonga aliwaagiza washukiwa hao kuhakikisha wanasalimisha nakala za vitambulisha vyao vya kitaifa kwa idara husika, kuripoti kwa Naibu Chifu wa eneo hilo mara mbili kwa wiki pamoja na kujisalimisha kwa maafisa wa upelelezi wa kesi hiyo mara moja kila baada ya wiki mbili.

Miili iliyofukuliwa katika kijiji cha Kwa Binzaro
Wakati huo huo upande wa mashtaka ukiongozwa na Naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma Jamie Yamina, uliomba kuwasilisha watu wengine wanne Mahakamani ikiwemo Jairus Otieno na mkewe Lilian Akinyi, Kahonzi Katana Karisa na Loise Zawadi waliojionda kama washukiwa na kugeuka kuwa mashahidi wa serikali.
Upande wa mashtaka pia uliaka kupewa siku 60 zaidi kuendelea kuzuiliwa kwa washukiwa wakuu Sherleen Temba Anido, James Kahindi Kazungu, Thomas Mukunwe na Kahidi Kazungu Garama katika kituo cha polisi cha Ngerenya, Kilifi, Watamu na Kijipwa ili kukamilisha uchunguzi wao kwani wanne hao wanakabiliwa na mashtaka ya itikadi kali, ugaidi, kujihusisha na uhalifu na kupanga mauaji.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Chrispus aomba msahama bunge la kaunti ya Taita Taveta

Mwakilishi wadi ya Bomani mjini Taveta kaunti ya Taita Taveta Chrispus Tondoo ameliomba bunge la kaunti hiyo msamaha kutokana na matamshi aliyoyatoa hapo awali akikashifu bunge hilo kwa madai ya kushamiri kwa visa vya ufisadi na utepetevu.
Tondoo akiomba msamaha katika bunge hilo alisema alitambua athari zilizosababishwa na matamshi hayo kwa wenyeji wa kaunti hiyo na bunge hilo, hali ambayo imemfanya kuchukua hatua hiyo ya kuomba msamaha.
Aidha Tondoo aliahidi kuliheshimu bunge hilo kwa mujibu wa kanuni na Sheria za bunge la kaunti ya Taita Taveta.
‘’Naomba msamaha kutokana na matamshi ambayo niliyatoa tarehe 2 na tarehe 3 mwezi wa Juni mwaka huu wa 2025 kwani hayakuwa yenye heshima kwa wenyeji wa Taita Taveta na bunge la kaunti’’, alisema Tondoo.
Tondoo alikuwa Mwakikishi wa wadi wa pili kuomba msamaha baada ya Mwakilishi wa wadi ya Kaloleni mjini Voi Ahmed Azari kuchukua hatua hiyo mwezi mmoja uliyopita.
Haya yalijiri baada ya kaimu spika wa bunge hilo Anselim Mwadime kuapa kuwachulia hatua za kisheria wanachama wanne wa bunge hilo, wawili wakiwa ni Tondoo na Azari ambayo tayari wameomba msamaha huku wawili wakiwa wamesalia bila kuomba msamaha.
Taarifa ya Janet Mumbi