News
Chengo, awahimiza viongozi wa Pwani kutumia nafasi zao vizuri

Mwakilishi wa wadi ya Tezo kaunti ya Kilifi, Thomas Chengo alitoa wito kwa viongozi wa Pwani kutumia nafasi walizo nazo katika uongozi wa Kenya Kwanza ili kuboresha kaunti za Pwani kimaendeleo.
Chengo ambaye pia ni Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kaunti ya Kilifi, alisema kuna viongozi wengi wa Pwani ambao wako serikalini na ikiwa watatumia fursa hiyo ipasavyo huenda wapwani wakanufaika zaidi kupitia miradi mbalimbali.
Kulingana na Chengo, hii ndio mara ya kwanza kwa wapwani kuwa na viongozi wengi serikalini na akasisitiza umuhimu wa ushirikiano ili kuliboresha eneo la Pwani kama maeneo mengine nchini.
“Nataka ijulikane kwamba hii sio ajali na ikiwa hatutashikana vizuri, tukatumia hii nafasi vizuri nafasi hii kujirudia tena sio rahisi’’, alisema Chengo.
Vilevile aliwashinikiza viongozi wa kaunti ya Kilifi kuwahudumia wenyeji na kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kunyoshea kidole cha lawama kwa masuala ambayo hayana manufaa.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Joho, awahimiza wakenya kujisajili katika “Boma Yangu”

Waziri wa Madini na Uchumi wa raslimali za bahari Ali Hassan Joho, aliwahimiza wakenya kujisajili katika mpango wa “Boma Yangu” ili kunufaika na nyumba za bei nafuu zinazojengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Joho alipongeza mradi huo wa serikali, akisema unalenga kuwaondoa wakenya kutoka kwenye makaazi duni na kuwapatia makaazi bora yenye hadhi na mazingira salama ya kuishi.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa baada ya swala ya Eid-ul-Adha, Joho aliwahimiza wakaazi wa eneo la Pwani kuchukua hatua za haraka kujisajili ili wasikose fursa hiyo muhimu ya kuboresha maisha yao.
“Kuna huu mradi unaitwa Affordable Housing, huu mradi mmeona umefanywa mahali kwingi sana na sai usajili wa ule mradi ambao utafanyika pale VOK eneo bunge la Nyali, nyumba 1,976 zitajengwa na mambo mengine, nawasihi kwa heshima kubwa sana waingie kwa Boma Yangu wajisajili”, alisema Joho.
Kwa upande wake Kamishna wa kaunti ya Mombasa Mohamed Nur aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kutuma maombi ya nafasi za ajira katika mpango wa kazi mtaani kwa vijana.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
KHRC: Wasichana elfu moja ni wajawazito, Lamu

Takribani wasichana elfu moja kaunti ya Lamu wameripotiwa kupata mimba za utotoni kati ya mwaka wa 2024/25 huku visa vingi vikichangiwa na dhulma za kingono na ndoa za mapema.
Kulingana na Masharika ya kutetea haki za kibinadamu la MUHURI pamoja na lile la Kenya Human Rights Commission, KHRC serikali imeshindwa kuwakabili kisheria wahusika huku waathiriwa ambao ni wasichana wadogo wakiendelea kuhangaika.
Takwimu kutoka kwa kamati ya jinsia kaunti ya Lamu, iliwasilisha kwa kamati ya kitaifa inayoangazia masuala ya dhulma za jinsia kuwa kaunti hiyo ilinakili visa zaidi ya 700 vya mimba za utotoni mwaka wa 2024.
Takwimu hioz pia ziliweka wazi kwamba visa vingine zaidi ya 200 viliripotiwa kati ya mwezi Januari na Mei mwaka huu wa 2025.
Kulingana na ripoti kutoka kwa baraza la kitaifa la kudhibiti magonjwa NSDCC ilieonysha kwamba wasichana wanarika zaidi ya 600 nchini walipata mimba mwaka 2023.
Taarifa ya Janet Mumbi