News
Chahale, aishutumu serikali kutokana na dhulma za kijinsia

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kutetezi haki za kibinadamu la International Justice Mission, IJM, Vincent Chahale ameishutumu serikali kwa kuzembea katika kukabiliana na dhulma dhidi ya wasichana na wanawake nchini.
Chahale alisema kwamba wasichana wadogo wamekuwa wakidhulumiwa kingono na wengi wao huishia kukosa haki.
Alirejelea kisa ambapo msichana wa umri wa miaka 17 kwa jina Farida Julius Changawa aliyeuawa kinyama kwa kudungwa kesu eneo la Msumarini kaunti ya Kilifi ambali alisema ni sharti serikali iwe ange katika kuhakikisha kwamba wasichana wanalindwa dhidi ya dhulma katika jamii.
“Kuna pengo katika jamii yetu ambapo wasichana wadogo wanaendelea kudhulumiwa bila kupata haki. Kesi kama ya Farida ni kesi ya kusikitisha sana na tutaifuatilia hadi pale familia yake itakapopata haki” alisema Chahale.
Akiunga mkono kauli hiyo, Aggrey Juma meneja msimamizi wa Shirika la international Justice Mission alisema serikali inapaswa kutilia mkazo suala la dhulma dhidi ya Wanawake akieleza kusikitishwa na mauaji ya kinyama aliyotekelezewa marehemu Farida Julius.
Wawili hawa waliyasema haya wakati wa mazishi ya mwendazake Farida yaliyofanyika eneo la Mavueni siku Jumamosi ya tarehe ya 21 mwezi Juni 2025.
Farida alipitia dhulma ya kubakwa akiwa na umri wa miaka 13 kudhulimiwa tena miaka minne baadaye ambapo aliishia kuuawa kwa kudungwa kisu hivi majuzi.
Marehemu aliacha mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miezi 9.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Serikali na Wadau wa mazingira wapanda miti, Sabaki

Serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na mashirika ya kimazingira kaunti ya Kilifi inaendeleza mpango wa upanzi wa miti ili kuboresha mazingira.
Kulingana na Katibu wa masuala ya vijana na uchumi bunifu nchini Fikirini Jacobs, mpango huo unalenga kurudisha hadhi ya taifa la Kenya katika viwango vya kimazingira.
Akihutubia Wananchi wakati wa zoezi la upanzi wa mikoko katika eneo la Sabaki kaunti ya Kilifi, Fikirini alibainisha kwamba kupitia zoezi hilo jumla ya Miche elfu mbili ya mikoko kutoka kwa serikali na mashirika ya uhifadhi wa Mazingira imepandwa katika eneo hilo.
“Tumepanga miti mingi sana, idara yetu ya vijana imetoa miche elfu na kupitia mashirika mengi hapa wametoa miche elfu kwa jumla tumepanda miti elfu mbili, asante sana kwani kwa kufanya hivyo unasaidia pakubwa”, alisema Fikirini.
Wakati huo huo ameihimiza wananchi kuzingatia suala la upanzi wa miti pamoja na kujiepusha na ukataji miti kiholela, akisisitiza haja ya wakaazi kulinda misitu ili kuiwezesha jamii kuwa mazingira bora.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Kindiki, ataka makubaliano kati ya serikali kuu na kaunti kutekelezwa

Naibu wa rais Prof. Kithure Kindiki ametaka makubaliano yote kati ya serikali za kaunti na ile ya kitaifa kutekelezwa kabla ya mwezi Disemba mwaka huu wa 2025.
Akizungumza katika makao yake ya Karen jijini Nairobi Jumatatu 23, Juni 2025, kwenye mkutano wa 27 kati ya serikali kuu na zile za kaunti kuhusu bajeti IBEC, Kindiki alisema kumekuwa na makubaliano ambayo yamekuwa hayafuatiliwi ili kutekelezwa.
Kindiki alisema serikali kuu imejitolea kuhakikisha serikali za kaunti zinafanikisha miradi mbalimbali na kuwataka maafisa wa serikali za kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana kwa majadiliano.
Wakati huo huo alisisitiza haja ya kutafuta suluhu la matatizo yanayoathiri utendakazi wa serikali za kaunti huku akipuzilia mbali uwepo wa mzozo wowote baina ya serikali kuu na zile za kaunti.
Taarifa ya Janet Mumbi.