News
Alubbe: Tutazuru kaunti za Pwani kushughulikia suala tata la ardhi

Mkurugenzi mkuu wa shirika la utetezi wa haki za ardhi nchini Kenya Land Alliance Faith Alubbe amesema wameanzisha mchakato wa kuzuru kaunti zote 6 za pwani kuangazia suala tata la mizozo ya ardhi.
Akizungumza mjini Kilifi, Alubbe alisema kwamba ukanda wa Pwani ni mojawapo ya maeneo humu nchini ambayo yamesheheni dhulma za kihistoria kwenye masuala ya umiliki wa ardhi.
Alubbe ambaye pia ni Wakili wa masuala ya ardhi alihoji kwamba mikakati yao katika mchakato huu ni kuhakikisha kuwa wapwani wanaelewa kwa kina haki zao kuhusiana na umiliki wa ardhi za kibinafsi lakini pia za kijamii.
“Kuna hazina ya ardhi ambayo ilibuniwa baada ya mswada kuhusiana na hazina hiyo kupitishwa. Rais William Ruto tayari aliwekeza fedha kwenye hazina hiyo ila idadi kubwa ya wakaazi wa pwani hawana ufahamu kuhusu hazina hiyo” alisema Alubbe.
Alubbe alisema kuwa watahakikisha kuwa wapwani wanapata hamasa za kutosha kuhusiana na suala hilo lakini pia haki zao za ardhi kwa jumla.
“Inaweza kuwa muhimu watu wa pwani kuambiwa kuhusu hii hazina, ili wakapate kuelewa ni vipi hazina hizi zinawahusu”, aliongeza Alubbe.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Serikali na Wadau wa mazingira wapanda miti, Sabaki

Serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na mashirika ya kimazingira kaunti ya Kilifi inaendeleza mpango wa upanzi wa miti ili kuboresha mazingira.
Kulingana na Katibu wa masuala ya vijana na uchumi bunifu nchini Fikirini Jacobs, mpango huo unalenga kurudisha hadhi ya taifa la Kenya katika viwango vya kimazingira.
Akihutubia Wananchi wakati wa zoezi la upanzi wa mikoko katika eneo la Sabaki kaunti ya Kilifi, Fikirini alibainisha kwamba kupitia zoezi hilo jumla ya Miche elfu mbili ya mikoko kutoka kwa serikali na mashirika ya uhifadhi wa Mazingira imepandwa katika eneo hilo.
“Tumepanga miti mingi sana, idara yetu ya vijana imetoa miche elfu na kupitia mashirika mengi hapa wametoa miche elfu kwa jumla tumepanda miti elfu mbili, asante sana kwani kwa kufanya hivyo unasaidia pakubwa”, alisema Fikirini.
Wakati huo huo ameihimiza wananchi kuzingatia suala la upanzi wa miti pamoja na kujiepusha na ukataji miti kiholela, akisisitiza haja ya wakaazi kulinda misitu ili kuiwezesha jamii kuwa mazingira bora.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Kindiki, ataka makubaliano kati ya serikali kuu na kaunti kutekelezwa

Naibu wa rais Prof. Kithure Kindiki ametaka makubaliano yote kati ya serikali za kaunti na ile ya kitaifa kutekelezwa kabla ya mwezi Disemba mwaka huu wa 2025.
Akizungumza katika makao yake ya Karen jijini Nairobi Jumatatu 23, Juni 2025, kwenye mkutano wa 27 kati ya serikali kuu na zile za kaunti kuhusu bajeti IBEC, Kindiki alisema kumekuwa na makubaliano ambayo yamekuwa hayafuatiliwi ili kutekelezwa.
Kindiki alisema serikali kuu imejitolea kuhakikisha serikali za kaunti zinafanikisha miradi mbalimbali na kuwataka maafisa wa serikali za kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana kwa majadiliano.
Wakati huo huo alisisitiza haja ya kutafuta suluhu la matatizo yanayoathiri utendakazi wa serikali za kaunti huku akipuzilia mbali uwepo wa mzozo wowote baina ya serikali kuu na zile za kaunti.
Taarifa ya Janet Mumbi.