News
Alshabab yauwa KDF watatu Lamu

Wanajeshi watatu wa Kenya wameuawa, huku wengine saba wakiwachwa na majeraha mabaya mwilini, baada ya gari walimokuwa wakisafiria kukanyanga kilipuzi eneo la Badaah, kaunti ya Lamu.
Naibu kamishna kaunti ya Lamu Mashariki George Kubai alisema wanajeshi hao walikuwa wakiwapeleka wenzao eneo la Sankuri kutoka Kiunga wakiwa kwenye gari jingine wakati gari lao lilipokanyaga kilipuzi hicho kilichozikwa ardhini.
Waliojeruhiwa wanapokea matibabu katika hospitali ya Kiunga huku vyombo vya usalama vikianzisha oparesheni kuwasaka magaidi waliotega kilipuzi hicho.
Kaunti ya Lamu imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya kigaidi yanayotekelezwa na mgaidi wa alshabab kutoka taifa jirani la Somalia.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mboko: Serikali lazima ikomeshe mauaji dhidi ya Wanawake

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko ameitaka serikali kuhakikisha inakomesha mauaji ya kiholela na unyanyasaji wa kingono dhidi ya Wanawake nchini.
Akizungumza na Wanahabari, Mishi alisema ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kuona Wanawake wakiendelea kuuawa kila uchao na katika mazingira ya kutatanisha pasi na hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Mbunge huyo aliitaka serikali kuongeza ufadhili kwa Muungano wa Wabunge Wanawake ili kuwawezesha kufanikisha kampeni ya kuhamasisha kwa umma dhidi ya ukatili wa kijinsia.
“Ni lazima visa kama hivi vikomeshwe, tumechoka na mauaji ya kila mara ya wanawake nchini na sisi pia tuko na haki ya kuishi na tunaiambia serikali kupitia bunge itenge pesa kupitia muungano wa wabunge wanawake ili kuelimisha jamii kuhusu kukomesha mauaji ya wanawake nchini”, alisema Mishi.

Mbunge wa Likoni na Wanawake wakipinga mauaji ya kiholela dhidi ya wanawake
Wakati huo huo aaliwataka maafisa wa usalama kushika doria kikamilifu hasa katika maeneo yanayokumbwa na visa vya ukatili dhidi ya wanawake huku akipendekeza mashirika yasiokuwa ya kiserikali kushirikiana na viongozi katika juhudi za kukomesha visa hivyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Christine: Wahudumu wa afya 1,340 wapokea mafunzo Taita Taveta

Serikali ya kaunti ya Taita Taveta kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa nyanjani ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao bila vikwazo.
Naibu Gavana wa kaunti ya Taita Taveta Christine Kilalo alisema kuwa kati ya wahudumu hao 1,340 asilimia 75 tayari wanaendelea na mafunzo katika ngazi tofauti.
Kilalo aliahidi kushirikiana na wahudumu hao licha ya changamoto zinazowakabili nyanjani.
“Wamekubali wakafundiashwa ili waweze kutoa elimu ya afya na waweze kusaidia jamii kwa mambo ya usafi na pia kusaidia katika kuwasilisha ujumbe za kiafya na pia wakipata wagonjwa waweze kuwatuma mahali wanaweza wakapata huduma za matibabu’’, alisema Kilalo.
Wakati uohuo alidokeza kuwa serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na serikali kuu wameweka mikakati ya kuhakikisha wahudumu hao wanalipwa fedha ambazo zitawasaidia kujikimu kimaisha pamoja na familia zao.
“Tulikubaliana kama taifa asilimi 50 ambayo ni elfu mbili mia tano inalipwa na serikali kuu na asilimia 50 ambayo ni elfu mbili mia tano inalipwa na serikali ya kaunti na kama serikali tunaemda kukamilisha malipo’’, aliongeza Kilalo.
Taarifa ya Janet Mumbi