News
Vijana wa Kaunti ya Kilifi Wajisajili kwa Kazi za Ughaibuni

Mamia ya vijana wamejitokeza katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi Kaunti ya Kilifi kutafuta usajili wa kazi za ughaibuni kama ilivyotangazwa na serikali.
Kulingana na serikali, eneo la Pwani limetengewa nafasi 3,500 za kazi za ughaibuni katika mpango wa ajira uliopewa jina “Kazi Majuu” ikiwepo kazi za kuendesha piki piki, ubawabu, vijakazi shambani pamoja na wahudumu nyumbani.
Wengi wa vijana waliojitokeza katika zoezi hilo wameeleza matumaini ya kubadili maisha yao iwapo watafanikiwa, wakidai maisha ya humu nchini yamezidi kuwa magumu.
Kulingana na Jilani Justin Mwarumba mmoja wa vijana hao wameasema serikali inafaa kuwahakikishia usalama wa pesa watakazotumia katika zoezi hilo huku wakishinikiza kuangazia upya suala la ulipaji mkopo kwa wasio na uwezo wa kugharamia zoezi hilo la usajali.
Hata hivyo Wanaharakati wa kijamii mjini Kilifi wakiongozwa na Birya Menza wanashinikiza serikali kuhakikisha inabuni nafasi za ajira hapa nchini badala ya mataifa ya ugaibuni ambako wakenya wengi wamekuwa wakipitia madhila mengi mikononi mwa waajiri.
Zoezi hilo litaendelea katika kaunti zaMombasa na Kwale.
News
Wanaosajiliwa Kwenye Mpango wa Kazi “Majuu” Waonywa.

Waziri wa Leba nchini Dakta Alfred Mutua amewaonya vijana waliopata nafasi za ajira ughaibuni dhidi ya kujihusisha na visa vya utovu wa nidhamu.
Akizungumza wakati wa zoezi la kusajili vijana kwenye mpango wa ajira za nje nchi maarufu Kazi “Majuu” katika kaunti ya Kwale, Waziri Mutua alitaja hatua hiyo kwamba huenda ikachangia kandarasi zao kufutiliwa mbali sawa na kukabiliwa kisheria.
Mutua alidokeza kwamba kuna baadhi ya vijana ambao tayari wamerejeshwa nchini kufuatia visa vya utovu wa nidhamu
“Unaskia unawashwa unataka kuandamana, unataka kuwa mwanaharakati, unataka kuchochea ingia ndege uje hapa wikendi moja uandamane kila mahali hiyo kitu ikutoke urejee kazini, kwa sababu ukienda kufanya huko maandamano unaharibia wakenya wengine, kuna watu waliandamana huko nchi tofauti tofauti, wakenya kumi na tano wengi wakasimamishwa, wakaregeshwa nyumbani, unaandamana kwa nchi nyengine wanauliza mbona mkenya anaandamana na mganda haandamani, mbona mtanzania haandamani”, alisema waziri Mutua.
Akizungumzia suala la utumizi wa dawa za kulevya, Waziri Mutua amewataka vijana hao kukomesha uraibu huo kwani hakuna taifa linaloshabikia matumizi ya dawa za kulevya.
“Hapa utafanyia ukaguzi wa kiafya kama umekuwa ukivuta bangi, madawa ya kulevya utaanguka, hata ukikataa kupatikana hapa ukifika ng’ambo utapatikana, kwa hivyo kama unataka kwenda ng’ambo achana na bangi bwana”,aliongeza waziri Mutua.
Zoezi hilo lililenga vijana 800 kaunti ya Kwale na 3,500 eneo la pwani kwa ujumla.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Waasi wa M23 wazidisha Mapambano, DRC

Mapigano mapya yamezuka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada ya Waasi wa kundi la M23 kufutilia mbali pendekezo la ahadi za hapo awali za kujiondoa katika maeneo wanayoyadhibiti huku wakilishtumu jeshi la Kongo kwa kuendeleza uchokozi.
Wakati hayo yakiarifiwa, mataifa jirani yanaendelea kijaribu kufufua mchakato wa kutafuta amani katika taifa hilo ambalo limetumbukia katika migogogo ya kiutawala. Inaarifiwa kwamba Watu wawili wameuawa kufuatia mashambulio yaliyotokea katika hafla ya Mazishi ya Mwanamuziki maarufu wa Kongo.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanapambana na waasi wanaoegemea upande wa serikali huku nchi za kikanda zikijaribu kuupa msukumo mpya mchakato wa kutafuta amani ambao umekuwa ukisuasua.
Waasi wa M23 wamefanikiwa kuiteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo tangu Januari huku maelfu ya vifo vikiripotiwa na mamia ya maelfu ya watu wakilazimika kuyakimbia makazi yao.
Mapigano hayo yanazidi kupamba moto licha ya juhudi za viongozi wa nchi za ukanda wa Kusini mwa Mashariki mwa Africa kuutanzua Mgogoro huo unaotishia kusambaa na kuwa vita vikubwa vya kikanda.
Taarifa ya Eric Ponda.