News
Fedha za Shule Kusambazwa kwa Wakati, Asema Migos

Waziri wa Elimu nchini Julius Migos amesema serikali imeweka mikakati muafaka ya kuhakikisha fedha za kusimamia shughuli za masomo zinasambazwa kwa wakati unaofaa shuleni.
Waziri Migos akisema tayari Wizara yake imefanya kikao na Wizara ya Fedha nchini kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kikamilifu.
Aidha amesema hatua hiyo ni muhimu kwani itahakikisha wanafunzi wanapata huduma bora za masomo na kwamba itawawezesha walimu wakuu kusimamia shughuli za masomo bila changamoto.
Akizungumza mjini Mombasa baada ya kufungua rasmi kongamano la walimu wakuu wa shule za upili za kitaifa na shule za kufunza watoto wenye mahitaji maalum, Waziri Migos amesema hatua hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya masomo.
Wakati huo huo amewahakikishia walimu wakuu kwamba ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu na wadau wa sekta ya elimu nchini utahakikisha masuala ya elimu yanaendeshwa vyema.
News
Ruku: Serikali kuajiri vijana laki moja kwa NYS

Serikali inalenga kuajiri zaidi ya vijana laki moja katika Shirika la huduma kwa vijana wa taifa NYS.
Waziri wa utumishi wa umma nchini Geoffrey Ruku amesema hatua hiyo itachangia kuboreshwa kwa huduma za umma sawa na kuhakikisha Shirika la NYS linakuwa nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika kaunti ya Machakos, Waziri Ruku amesema hatua hiyo itapunguza utegemeaji wa ufadhili wa umma kwani shirika hilo itapanua mikakati bora ya serikali ya kibiashara pamoja na kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Ruku amelishinikiza bunge la kitaifa kuharakisha marekebisho ya mswada wa NYS ambao utawalishwa na Wizara yake bungeni ili kusawazisha mfumo wa kisheria wa shirika hilo.
Wakati huo huo amewataka vijana kukumbatia mipango ya serikali ya kujumuisha wananchi wote pamoja katika kufanikisha ajenda ya serikali ya maendeleo endelevu hadi mashinani.
News
Nyakang’o, apendekeza mgao wa shilingi bilioni 1.6

Mdhibiti wa bajeti nchin Margaret Nyakang’o amependekeza kuongezwa kwa kiwango cha bajeti ya ofisi yake kutoka shilingi milioni 7.2 hadi shilingi bilioni 1.6 ili kufanikisha majukumu yake.
Akizunguza mjini Mombasa wakati wa kikao na kamati ya uekezaji wa umma na hazina maalum katika bunge la Seneti, Nyakang’o amesema bajeti hiyo ya ofisi yake iko chini mno katika kufanikisha mikakati endelevu ya majukumu yake ya kikazi.
Hata hivyo amesema iwapo bajeti hiyo itaongezwa ofisi yake itakuwa na wakati mwafaka wa kukagua miradi ya maendeleo katika kaunti zote nchini.