National News
Wanaharakati Kilifi Waishinikiza Serikali ya Kitaifa Kumaliza Ujenzi wa Daraja la Baricho

Wanaharakati wa kijamii katika kaunti ya Kilifi wameishinikiza serikali ya kitaifa kukamilisha mradi wa ujenzi wa daraja la Baricho katika gatuzi dogo la Magarini ili kuboresha shughuli za uchukuzi na biashara.
Wakiongozwa na Kenza Ondieki, Wanaharakati hao wamesema ujenzi wa daraja hilo umechukua muda mrefu huku wenyeji wa eneo hilo wakiendelea kuathirika kiusafiri.
Ondiek amedokeza kwamba kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa za kilimo hadi sokoni sawa na kuimarisha uchumi wa eneo hilo.
Kwa upande wake Mbunge wa zamani wa Magarini Joseph Kasena Yeri amekariri kwamba kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia wakaazi wengi wa Magarini wanaotafuta huduma muhimu mjini Malindi kuzipata kwa urahisi.
National News
Chonga: Wakenya Wanaosafiri Ughaibuni Kusaka Ajira Hawazingatii Sheria za Leba

Mwenyekiti wa kamati ya Leba katika bunge la kitaifa Ken Chonga amesema baadhi ya wakenya ambao wanasafiri katika mataifa ya miliki za kiarabu kusaka ajira wamekosa kuzingatia sheria za Wizara ya Leba nchini na kuangukia mikononi mwa walaghai.
Chonga amesema ni lazima wakenya hao wachunguze mawakala wanaowasafirisha katika mataifa hayo kama wanatambulika na serikali, ndipo waingie katika mikataba ya uajiri ambayo imezingatia sheria za Leba nchini.
Akizungumza na Wanahabari mjini Kilifi, Chonga ambaye pia ni Mbunge wa Kilifi Kusini amesema ili wakenya waepuke madhila mbalimbali kutoka kwa waajiri wao katika mataifa hayo ni lazima wasafirishwe na mawakala waliosajiliwa na serikali.
Wakati huo huo amesema japo serikali iko mbioni kuhakikisha inawatafutia wakenya kazi katika mataifa ya ughaibuni ni lazima wanaosaka ajira za ughaibuni waingie katika mkataba wa uajiri kabla ya kusafiri nje ya nchi.
National News
Chibule: Visa vya Dhulma za Kijinsi Vimepungua Kilifi

Serikali ya kaunti ya Kilifi imesema visa vya dhulma za kijinsia katika kaunti hiyo vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Kulingana na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Flora Mbetsa Chibule, visa hivyo viliongezeka zaidi msimu wa maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo kaunti ya Kilifi iliorodheswa nafasi ya tatu nchini baada ya kaunti ya Bungoma na Samburu.
Chibule amesema kwa sasa ni asilimia 12.3 pekee ya visa hivyo vilivyoripotiwa tofauti na asilimia 30 wakati wa maambukizi ya Corona, akisisitiza kwamba juhudi hizo zimefanikiwa kupitia ushirikiano wa jamii na wadau mbalimbali.
Kiongozi huyo amedokeza kwamba serikali ya kaunti imetoa mafunzo kwa maafisa wa kutoa ushauri nasaha ili kusaidia kupambana na visa hivyo mashinani, akisema juhudi hizo zitaendelezwa sawa na kudhibiti madhila hayo.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba kaunti hiyo imekamilisha ujenzi wa sehemu salama ya kuwahifadhi watoto wanaopitia dhulma za kijinsia wakati kesi zao zikiendelea Mahakamani.