News
Wanaharakati Waitaka Serikali Kuongeza Muda wa Kuvifanyia Vipimo vya DNA Familia Zilizopoteza Zilizofiwa Shakahola

Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu katika eneo bunge la Malindi na Magarini kaunti ya Kilifi wanaitaka serikali ya kitaifa kuongeza muda wa kuvifanyia vipimo vinasaba yani DNA za familia zilizopoteza wapendwa wao katika msitu wa Shakahola.
Wakiongozwa na Thomas Karisa, Wanaharakati hao wamesema miili mingi iliyofukuliwa katika makaburi ya msitu wa Shakahola haijatambuliwa hali ambayo imeziacha familia zilizowapoteza wapendwa wao kusalia katika njia panda.
Karisa ameitaka serikali kuikabidhi miili iliyotambuliwa kwa familia husika kwa ajili ya maandalizi ya mazishi na pia kuchukua jukumu la kuizika miili ambayo haitatambulika hata baada ya kukamilika kwa muda wa uchunguzi.
Kwa upande wake Stephen Mwiti ambaye alipoteza watoto wake 5 katika msitu wa Shakahola amesema amepoteza matumaini ya kuipata miili ya wanawe licha ya kufanyiwa vipimo vya DNA tangu mwaka uliopita.
News
Kadinali Bacciu Atangaza Kutohudhuria Kikao cha Conclave

Kadinali Giovanni Angela Bacciu ametangaza kujiondoa katika kikao cha siri cha kumchagua Papa mpya kilichopangwa na Ofisi ya Vatican kuanza rasmi mwezi Mei 7.
Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia Wakili wak siku ya Jumanne tarehe 29, Kadinali Bacciu amesema ameamua kutii wasia ulioweka wa Hayati Papa Francis ingawa alidumisha kutokuwa na hatia.
“Kwa kuwa moyoni mwangu nina wema wa Kanisa ambalo nimelitumikia na nitaendelea kulitumikia kwa uamunifu na upendo na kuchangia ushirika na utulivu wa Conclave, nimeamua kutii kama nilivyofanya siku zote wakati wa Papa Francis na nitasalia kuamini kwamba sina hatia”, alisema Kadinali Bacciu.
Kadinali Bacciu mwenye umri wa miaka 78 na mzaliwa wa taifa la Italia amegongwa vichwa vya habari kutokana na msimamo wake huku baadhi ya wachanguzi wakisema uamuzi wake umetokana na sintofahamu zilizokuwepo kati yake na Hayati Papa Francis mwaka wa 2020 baada ya kuagizwa na Papa Francis kujiuzulu kwa kupatikana na kashfa ya ufisadi.
News
Mbogo: Kaunti ya Mombasa Imeshindwa Kutatua Mzozo wa Ardhi

Aliyekuwa mbunge wa Kisauni Ali Mbogo ameikosoa serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kushindwa kutatua suala tata la uskwota linalowakumba wakaazi wengi wa kaunti hiyo.
Akizungumza katika eneo la Kisauni katika kaunti ya Mombasa, Mbogo amesema tatizo la uskwota limeendelea kuwa chanzo kikuu cha migogoro ya ardhi na ukosefu wa usalama katika maeneo mengi ya kaunti ya Mombasa huku serikali ya kaunti hiyo ikionekana kulifumbia macho suala hilo.
Mbogo amedai kwamba maelfu ya wakaazi wa Kisauni na Mombasa kwa jumla wanaishi kwa hofu ya kufurushwa katika ardhi zao walizoishi tangu jadi kufuatia ukosefu wa hati miliki.
Wakati huo huo amedokeza kwamba baadhi ya maafisa wa serikali ya kaunti hiyo wanahusishwa na visa vya uporaji wa ardhi za umma kwa kushirikiana na waekezaji jambo ambalo amelitaja kuwa dhulma.